Newcastle kuizamisha Arsenal Jumamosi

Muktasari:

  • Fernandez alisema baada ya kupoteza michezo mitatu ya mwanzo katika Ligi Kuu msimu huu hawatarajii tena kupoteza mechi zijazo kwani wameshajua wanapokosea.

London, England. Mlinzi wa kati wa timu ya Newcastle United raia wa Argentina, Federico Fernandez, ametamba kuwa wataifunga Arsenal katika mchezo wa Ligi Kuu England utakaopigwa Jumamosi hii.

Fernandez alisema baada ya kupoteza michezo mitatu ya mwanzo katika Ligi Kuu msimu huu hawatarajii tena kupoteza mechi zijazo kwani wameshajua wanapokosea.

Alisema kuwa wachezaji wote wamejiapiza kutoruhusu pointi kuondoka kwenye dimba lao la St James’s Park, badala yake wamepanga kuzishinda timu zote zitakazotua kwenye dimba hilo ili kuwalipa fadhila mashabiki wao.

Newcastle inayonolewa na kocha mzoefu, Rafa Benitez, iko nafasi ya tatu kutoka mkiani mwa ligi baada ya kufungwa mechi zote tatu za kwanza dhidi ya mabingwa watetezi, Manchester City, Chelsea na Tottenham Hotspur.

“Hatuwezi kukubali kufungwa na Arsenal Jumamosi hii kwa sababu tutakuwa nyumbani St James Park, tunataka kushinda na kupata pointi tatu za kwanza, tumejizatiti licha ya kujilinda lakini tutashambulia kwa muda wote wa mchezo,” alisema.

Mchezaji huyo aliyesajiliwa kiangazi cha mwaka huu akitokea Swansea City, ameshaichezea mechi mbili na ametamba kuwa walifungwa na timu zenye ubora mkubwa ukilinganisha na Arsenal.

“Hatufurahii kuanza vibaya Ligi ya msimu huu, lakini tunajiliwaza kwa sababu tumecheza na timu vigogo ambazo zina uwezo mkubwa kwa sasa kila mmoja anaklijua hilo, lakini baada ya hapo hatutarajii tena kupoteza pointi,” alisema Fernandez.

Alisema wanajilaumu kwa kushindwa kupata pointi moja walipocheza na Cardiff City mchezo ambao walimalizwa na penalti waliyopata wapinzani wao dakika ya mwisho wa mchezo huo na kuzaa bao.

Kwa upande wa Arsenal ambayo inacheza msimu wake wa kwanza bila ya uongozi wa Kocha Arsene Wenger, mrithi wake Unai Emery, bado haijaonyesha kitu kipya.