Neymar apiga bao la ‘usiku’ PSG

Muktasari:

  • Mchezaji wa kimataifa wa Brazil, Neymar amefunga bao la dakika za lala salama katika mchezo ambao PSG ilishinda dhidi  ya Lyon.

Paris, Ufaransa. Mshambuliaji nyota wa Paris Saint Germain (PSG), Neymar amefunga bao la ‘usiku’ lililoipa timu hiyo pointi tatu muhimu.

PSG ikiwa ugenini ilishinda bao 1-0 dhidi ya Lyon katika mchezo wa Ligi Kuu Ufaransa.

Neymar alifunga bao kwa kiki ya mguu wa kushoto zikiwa zimebaki dakika tatu kabla ya mpira kumalizika.

Awali, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Brazil,  alifunga bao dakika ya 92 katika mchezo wa mwishoni mwa wiki iliyopita dhidi ya  Strasbourg.

Neymar amerejea katika ubora wake baada ya kukosa mechi tano tangu alipoibua mjadala wa kutaka kurejea Barcelona katika usajili wa majira ya kiangazi kabla ya mpango huo kukwaa kisiki.

Barcelona iliwahi kumpandia ndege Neymar kumfuata Paris kwenda kumalizana, lakini klabu hiyo iliweka ngumu ikitaka zaidi ya Pauni200 milioni.

Lakini, jana alirejea katika ubora wake baada ya kukosa mechi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya walioshinda mabao 3-0 dhidi ya Real Madrid.

Mshambuliaji huyo anarejea uwanjani baada ya kuwatibua   mashabiki wa klabu hiyo tangu alipoweka bayana azma ya kutaka kurejea Barcelona. Nyota huyo amefunga mabao 36  katika mechi 39 alizocheza PSG.