Neymar arejea PSG kupunguza munkari

Muktasari:

Mshambuliaji huyo Mbrazili amekuwa kwenye mzozo na klabu yake kuhusu majibu yake kwa vyombo na habari na pia tetesi za uhamisho wa kurejea Barcelona.

 

Neymar leo Jumatatu ameibuka katika mazoezi ya klabu yake ya Paris Saint-Germain kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ufaransa, akiwa amechelewa kwa wiki nzima na ikiwa ni siku chache baada ya kuikera klabu hiyo kwa kuwa kumbukumbu yake nzuri ni wakati alipoichezea Barcelona na kuishinda PSG.

PSG ilianza mazoezi Jumatatu iliyopita lakini Neymar, ambaye anahusishwa na uhamisho kurejea Barcelona, amewasili wiki moja baadaye kwa mujibu wa klabu hiyo, wakati nyota huyo anasisitiza kuwa alishakuwa na makubaliano ya kuchelewa kambini.

PSG ilimjibu wiki iliyopita kwa kutishia kuchukua "hatua sahihi" dhidi ya mchezaji huyo ghali duniani ambaye alisema aliendelea kubakia nchini Brazil kwa ajili ya kuhudhuria mashindano ya hisani ya timu za wachezaji watano kila upande yanayoendeshwa na taasisi yake ya hiari inayoitwa Neymar Institute.

Jumamosi, nyota huyo mwenye umri wa miaka 27, ambaye alijiunga PSG kwa ada ya dola 250 milioni mwaka 2017, ametoa matamshi kadhaa ambayo yameharibu uhusiano wake na klabu hiyo na kuzua mtafaruku kwenye mitandao ya kijamii.

Alipoulizwa na chaneli ya michezo mtandaoni ya Oh My Goal kuhusu kumbukumbu yake nzuri, mshambuliaji huyo alisema ni ya ushindi wa aina yake wa Barcelona wa mwaka 2017 wakati alipokuwa kwenye kikosi kilichoilaza PSG mabao 6-1 na kufanikiwa kupindua ushindi wa wababe hao wa Paris wa mabao 4-0 katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa.

Mapema leo, Neymar alituma mtandaoni video ya sekunde 10 inayomuonyesha akiwa amevalia jezi ya Barcelona na nukuu ya katika Biblia inayosema  "hakuna silaha dhidi yako itakayofanikiwa".