Ni zamu yetu Afcon

Muktasari:

Ushindi au sare na ushindi wa Cape Verde vitafungua njia ya Tanzania kucheza fainali za Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39 iliyopita.

Dar es Salaam.’Afcon ni Zamu Yetu’, ndivyo wachezaji wa Taifa Stars watakavyoingia uwanjani wakiwa na neno hilo kichwani mwao pale watakapoikabili Uganda katika mchezo wa mwisho wa Kundi L kutafuta nafasi ya kufuzu Fainali za Afrika (Afcon) mwaka huu.

Hakuna kingine zaidi ya Taifa Stars kushinda mchezo huo lakini pia kukazia maombi yote kwa Cape Verde iifunge Lesotho au itoke nayo sare tu ili Tanzania iandike historia nyingine ya kucheza Afcon kwa mara ya pili tangu ilipofanya hivyo mwaka 1980.

Licha ya Uganda kuwa tayari imeshafuzu Fainali hizo lakini ni wazi haitakuwa tayari kufungwa kirahisi huku kipa wake Dennis Onyango akitaka kuendeleza rekodi yake ya kutoruhusu bao lolote tangu kuanza kwa mashindao hayo hadi fainali.

Ushindi au sare na ushindi wa Cape Verde vitafungua njia ya Tanzania kucheza fainali za Afrika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 39 iliyopita.

Hivyo Taifa Stars itatakiwa kujipanga hasa na kucheza kwa nidhamu, akili na kujitolea na kuhakikisha inapata ushindi. Taifa Stars inashika nafasi ya tatu kwenye kundi L ikiwa na pointi tano sawa na Lesotho iliyo nafasi ya pili. Uganda inaongoza kundi ikiwa na pointi 13 wakati Cape Verde inashika mkia ikiwa na pointi nne.

Hata hivyo, timu zote tatu, Tanzania, Uganda na Cape Verde zina nafasi ya kusonga mbele kutegemeana na matokeo ya mwisho baada ya dakika 90.

Mashambulizi mwanzo mwisho

Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike ni kama amejipanga kwa soka la kushambulia mwanzo mwisho kutokana na jinsi alivyokuwa akifanya katika mazoezi ya timu yake.

Katika mazoezi yaliyofanyika jana asubuhi kwenye Uwanja wa Boko Veterani kocha huyo raia wa Nigeria alionekana kuwaelekeza wachezaji wake kutumia vizuri mipira ya kona na faulo za moja kwa moja.

Zoezi hilo lilifanyika vizuri hasa katika mipira ya faulo ingawa katika kufunga kwa mipira ya kona ilionekana bado tatizo kwa wachezaji wengi.

Amunike alianza na zoezi la kufunga kwa kutumia mipira ya kona na aliwapanga washambuliaji wote pamoja na mabeki na Shiza Kichuya kupiga kona kutokea upande wa kulia huku Mudathir Yahaya akipiga kona kutokea upande wa kushoto.

Hata hivyo, licha ya Kichuya na Mudathir kupiga kona nzuri lakini wachezaji wengi wa Taifa Stars hasa washambuliaji walishindwa kuzitumia vizuri hivyo mara kwa mara Amunike kusimamisha mazoezi na kuwapa maelekeza.

Baadaye kocha huyo aliwapanga Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, Saimon Msuva na Shiza Kichuya katika sehemu ya kupiga mipira ya faulo ya moja kwa moja nje kidogo ya 18 huku golini kipa akiwa Metacha Mnacha waliokuwa wakibadilishana na Aaron Kalambo wakilindwa na ukuta uliowekwa na Rashid Mandawa, Himid Mao, Kennedy Juma na Feisal Salum.

Hata hivyo kundi la wachezaji lililoongozwa na nahodha Samatta lilionekana kushindwa kutumbukiza mpira wavuni mara nyingi kwa mipira ya faulo,wengi wakipaisha au wakipiga nje na mingine ikigonga ukuta wa mabeki.

Samatta na Msuva walifunga mara mbili kati ya mara nne walizopiga faulo hizo. Wachezaji hao ndio wanatarajiwa kuongoza mashambulizi ya Taifa Stars.

Manula, Yondani wazua hofu

Kipa Aishi Manula na Kelvin Yondani wamezua hofu kama watakuwemo katika mchezo wa leo licha ya Dakrati wa Taifa Stars Richard Yomba kuwatoa hofu Watanzania.

Manula na Yondani walishindwa kufanya mazoezi na wenzao hivyo kuzua wasiwasi kama watakuwa fiti kwa mchezo wa leo dhidi ya Uganda. Manula hakuwepo kabisa mazoezini wakati Yondani alikudhuria mazoezi hayo lakini alikaa nje ya uwanja akipatiwa matibabu. Yomba alisema Manula ameshindwa kufanya mazoezi kwa sababu ameenda hospitali baada ya kushtua mkono wakati Yondani ana maumivu ya mguu wa kulia.

“Manula ameshtua mkono na ukawa unamuuma hivyo amepelekwa Hospitali(jana) ili kuangaliwa lakini kesho( leo) dhidi ya Uganda ninaamini atakuwa vizuri na anaweza kucheza.

“Yondani alishtua mguu wake wa kulia hivyo ikabidi tumpumzishe mazoezi ili kumpooza na barafu lakini naye anaendelea vizuri”alisema Yomba.

Mshambuliaji wa Taifa Stars, Saimon Msuva alisema: “Afe kipa afe beki, leo ushindi lazima.

“Tunashukuru kuona wachezji wote tuna ari kubwa ya ushindi, tumefanya mazoezi vizuri tayari kwa mchezo huo,yaani lolote litokee ushindi lazima Jumapili(leo). Tuko tayari. Nakwambia Afcon ni Zamu yetu,” alisema Msuva.

Mukebezi anena

Leopold Taso Mukebezi aliyekuwemo kikosi cha Taifa Stars kilichocheza Lagos 1980, amewataka wachezaji wa timu hiyo kuhakikisha wananapata goli ndani ya dakika 10 za mwanzo ili kurahisisha safari.