Ninja: Kombe la FA ni tiketi ya Yanga kimataifa

Muktasari:

Yanga imeshauriwa kuelekeza nguvu katika mashindano ya Kombe la FA ili kupata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika mwakani.

Dar es Salaam.Beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu 'Ninja' anaamini timu hiyo ina nafasi kubwa ya kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani kwa kuhakikisha inatwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho Azam (ASFC).

Yanga leo itacheza mechi yake ya hatua ya 16 bora ya kombe hilo dhidi ya Gwambina FC kwenye Uwanja wa Uhuru.

Akizungumzia nafasi ya Yanga kucheza mashindano ya kimataifa mwakani, Ninja alisema wachezaji wanatakiwa kujituma na kufanya vizuri katika Komba ASFC.

“Sina maana kwamba wachezaji wakose nguvu yakujitoa kupamba katika mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, isipokuwa waone wapi wana nafasi kubwa ya kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya kimataifa.”

"Ligi bado ingawa kwa haraka haraka Simba inaonekana kama ina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa kutokana na pointi wanazomiliki ingawa mechi bado zipo nyingi ambazo zinaweza zikabadilisha upepo,"

"Wakati Yanga inapambana katika ligi pia isisahau kuweka nguvu Kombe la FA ambako inaweza ikapata nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa ingawa na kwenye kuna ushindani wa hali ya juu," alisema Ninja.