Nyota wa Kagera Sugar, Behewa afariki dunia

Muktasari:

 

  • Behewa aliwahi kuzichezea timu za Njombe Mji na Kagera Sugar mpaka umauti unamkuta.

Dar es Salaam. Wakati watanzania wakiwa wanasubiri kuona namna ambavyo Taifa Stars inawatoa kimasomaso katika mchezo wao dhidi ya Uganda, Taifa limeingia katika msiba baada ya kiungo wa Kagera Sugar, Behewa Sembwana kufariki leo alfajiri.

Kiungo huyo alifariki baada ya kusumbuliwa na maumivu ya tumbo kwa muda mrefu, hali ambayo ilimlazimu kufanyiwa operesheni takribani mara mbili.

Baada ya Mwanaspoti kupata taarifa za msiba huo zilimtafuta nahodha wa Kagera Sugar, George Kavila ambaye alithibitisha taarifa za kifo cha mchezaji huyo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Kavila alisema kweli mchezaji wao amefariki baada ya kusumbuliwa na maumivu ya tumbo ambayo alianza kulalamika tangu wakiwa pamoja kikosini.

“Nakumbuka alianza kuumwa wakati tunacheza na Mwadui, alishindwa kutoka na sisi kwenda kule Complex baada ya hapo alipelekwa hospitali alipatiwa matibabu, lakini baadaye alihamishiwa Muhimbili ndio mauti yakamkuta akiwa hapo,” alisema.

Aliongeza kwamba mchezaji huyo ameondoka akiwa na umri mdogo licha na alikuwa amebarikiwa kipaji hasa katika kuuchezea mpira anapokuwa yupo uwanjani.