Nyota wapya wampa mzuka Tshishimbi

ACHANA na matokeo ya mchezo wa jana Jumatano kati ya Yanga na Kagera Sugar, nahodha wa Yanga, Papy Kabamba Tshishimbi ameibuka na kuupongeza uongozi wao kwa kufanya usajili matata kwenye dirisha dogo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Tshishimbi amesema ujio wa nyota wapya waliosajiliwa dirisha dogo, umeongeza uhai na kuziba nafasi zilizoachwa wazi huku akiweka wazi kwamba, nafasi ya kufanya kweli iko wazi na msimu ujao watashiriki michuano ya kimataifa.

Alisema kulikuwa na kina Juma Balinya, Issa Bigirimana, Mayben Kalengo, David Molinga na nyota wengine baada ya kutimuliwa kwao hakuna kinachokumbukwa kutokana na kutua kwa nyota wapya wakali zaidi.

“Usajili uliofanya unahitaji kutoa pongezi kwa viongozi kwani wamefanya kitu ambacho kimerudisha heshima ya klabu wachezaji waliosajiliwa hasa waliopata nafasi ya kucheza kama Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima, Adeyum Salum na Tariq Seif wameonyesha viongozi hawakukosea kuwasajili.

“Tunatakiwa kuwapa muda, nategemea watafanya kitu kikubwa zaidi kikubwa ni uongozi kuendelea kuwatengenezea mazingira mazuri ili waendelee kufanya vitu bora zaidi na kuweza kuifanya timu ikiwapa changamoto wapinzani wetu kwenye kila mashindano tutakayoshiriki,” alisema.

Tshishimbi aliongeza kwa kuzungumzia suala la kocha mpya Luc Eymael ambapo alifunguka kuwa ujio wake umeongeza changamoto ya wachezaji kupambana lengo likiwa ni kuonyesha nini wanacho ili kujitengenezea mazingira ya kupata namba kikosi cha kwanza.

“Unajua tupo chini ya kocha mpya, hivyo changamoto iliyopo sasa ni kila mchezaji kuonyesha nini anacho ili kumshawishi mwalimu aweze kumuamini na kumpa namba kikosi cha kwanza chachu hiyo pia naamini itaongeza ushindani ndani ya klabu kwani kila mmoja atataka kufanya vizuri pale anapopata nafasi ya kucheza,” alisema.

Alisema kwa muda waliokaa naye na kuwasimamia mazoezi ameona vitu vingi vizuri kutoka kwa wenzake, hivyo anaamini ni mwanzo mzuri ambao utaifanya Yanga iwe timu bora na ya ushindani huku akiweka wazi kuwa mpira unachezwa sehemu ya wazi anachokizungumza kila mmoja atakiona.