Nyuma ya Pazia: Kompany ametamani mapema kuwa Pep

Saturday May 25 2019

 

By Edo Kumwembe

WAKATI fulani hivi Aprili. Alizaliwa Mwanafasala William Shakespeare. Wakati fulani Aprili alizaliwa Julius Nyerere. Alizaliwa pia Eddie Murphy. Alizaliwa pia Saddam Hussein. Alizaliwa pia Vladimr Lenin. Nilizaliwa pia mimi. Ndio, usicheke.  
Na mmoja kati ya watu waliochelewa kuzaliwa katika mwezi huo wa April ni huyu Vincent Kompany. Alizaliwa pale Brussels eneo la Uccle Aprili 10, 1986. Ana miaka 33 tu. Bado mdogo tu kwa chochote ambacho unaweza kusema.
Katika soka, pale Man City, anaweza kuonekana mzee. Kisa? Pep Guardiola ameiweka timu katika kiwango cha juu. Anapokosekana bado timu inafanya maajabu.
Anapokuwepo bado timu inafanya maajabu. Sio yeye tu, kuna wachezaji wengi wakikosekana bado wengine wanapiga mwendo mdundo. Wiki iliyopita Kompany ameondoka kurudi kwao Ubelgiji. Kule ndiko alikoibukia kisoka akiwa na Anderlecht. Amerudi tena Anderlecht baada ya kuondoka miaka 13 iliyopita. Akapita Ujerumani kisha akaenda zake City.
Sina shaka na heshima ya Kompany. Mwili wake unanuka mataji aliyobeba City. Majuzi mashabiki wa City walikuwa wanapitisha karatasi ya kuomba saini za mashabiki wapige kura za kuweka mnara wa heshima wa Kompany pale Etihad.
Sina tatizo. Wamechukua mataji sita ya England katika historia yao na kati ya hayo manne yamebebwa na Kompany.
Kinachonishangaza ni namna ambavyo katika umri wa miaka 33 Kompany kaamua awe kocha mchezaji. Anakwenda Anderlecht akiwa kocha zaidi pengine kuliko kuwa mchezaji. Kompany huyuhuyu ambaye ni bora kuliko Shokdran Mustafi au Chris Smalling? Nashangaa kidogo.
Sawa, Kompany anasumbuliwa na majeraha ya mara kwa mara, lakini ni bora uwe na Kompany anayecheza mechi 15 za ligi kuliko Smalling au Mustafi anayecheza mechi zote 38 za ligi. Huu ndio ukweli ambao inabidi tuumeze.
Kompany amewahi kurudi kwao. Angeweza kwenda huku na kule kabla hajarudi Anderlecht akiwa na miaka 37 na kuwa kocha mchezaji kwa msimu mmoja kabla ya kustaafu. Kuna safu nyingi za ulinzi katika timu kubwa Ulaya ambazo ni mbovu na Kompany angeweza kucheza bila shida. Tatizo ni hamu yake ya kuwa kocha. Nadhani baada ya kukaa na Pep Guardiola kwa misimu kadhaa amenogewa na sasa anataka kuwa Pep mwingine.
Walio karibu na Pep wanadai ‘Pep anakutia hamu uwe kocha’. Jinsi anavyowasoma wapinzani, jinsi anavyowapa mbinu wachezaji wake, mwishowe anavyoshinda mechi katika njia zilezile alizowatuma, inakufanya uwe na hamu ya kuwa kocha. Yaani unaona rahisi kufanya kama yeye. Nadhani Kompany naye ameingia katika mkumbo huu.
Kwa sasa kuna kizazi kipya cha makocha kinachotaka kuingia na kuwafanya kina Jose Mourinho kuwa wazee zaidi. Achana na kizazi cha kina Zinedine Zidane, Mauricio Pochettino, Jurgen Klopp, Pep mwenyewe na Diego Simeone, naona kuna kizazi kingine kinakuja kwa nyuma.
Kizazi hiki kina hawa kina John Terry, Patrick Vieira, Frank Lampard na Steven Gerrard. Hawa wanaingia miaka 40 na michache juu yake, na wale kina Pep na wengine wanaribia miaka 50. Kompany ametamani kwenda sawa na hawa kina Terry ingawa yeye amepata tamaa mapema zaidi.
Angeweza kutupa burudani tena kwa misimu miwili mitatu akiwa na Tottenham, au Arsenal, au Bayern Munich. Anataka kwenda kujikomaza katika kazi pale kwao anakoabudiwa, halafu arudi England kuchukua timu.
Hata hivyo, haishangazi. Mabeki wa kati pamoja na viungo wakabaji wanaipenda sana hii kazi ya ukocha. Franz Beckenbauer, Simeone, Guardiola, Pochettino, Gennaro Gattuso, Antonio Conte na wengineo wengi hawa ama walikuwa mabeki wa kati au viungo wakabaji.
Wanautazama mpira kwa mapana wakiwa uwanjani. Haishangazi kuona wakiwa manahodha katika timu zao. Wote hawa, kasoro Pep walikuwa manahodha. Wanawarekebisha wenzao, wanautazama uwanja katika mapana yake wakati mechi ikiendelea. Wakati soka lao linapokaribia kuisha wanageukia ukocha.
Tatizo langu liko palepale, Kompany amewahi sana. Kutoka Ligi Kuu ya England ukiwa nahodha wa Manchester City na ghafla kurudi Anderlecht inakuwa safari ya ghafla. Hakushuka taratibu. Kutoka katika lile shuti dhidi ya Leicester City kisha mechi tatu baadaye unarudi Brussels, inaonekana amepanga safari ya ghafla.
Kila la kheri anakokwenda. Tunawakaribisha makocha wengi wapya wenye changamoto mpya. Hasa katika nyakati hizi ambazo unaona wazi hata kina Mourinho wenyewe wameanza kupitwa na wakati. Wanaishia kuzurura tu katika vyombo vya habari baada ya kuziparaganyisha timu kubwa kama Chelsea, Liverpool  na Manchester United ambayo ilibamba kinoma.

Advertisement