Nyuma ya pazia bifu la Man United, Liverpool

LIVERPOOL, ENGLAND. KAMA kuna kitu mashabiki wa Manchester United wanakichukia basi ni mafanikio ya Liverpool, lakini pia kama kuna kitu kinawapa raha watu wa Anfield ni majanga ya Old Trafford.

Unaambiwa Liverpool na Man United zinachukiana kinoma yaani na siku zote zinaombeana njaa kwa sababu bifu lao linatoka mbali sana ni zaidi ya soka. Hivyo, wakati Liverpool ikitaka kutumia pambano la leo kuendelea kuandika rekodi kwenye Ligi Kuu England, Man United watafanya kila wawezalo kuhakikisha wanazuia hilo lisitokee.

Maana furaha ya Liverpool ni kilio kwa Man United na hiki ndicho kinafanya pambano la leo kuwa la kipekee na lenye upinzani mkali mkubwa.

Upinzani wa Manchester Dabi (Man United vs Manchester City), au Merseyside Dabi (Liverpool vs Everton) haufikii huu wa Man United na Liverpool maana kwa ufupi huu ni zaidi ya upinzani ni chuki.

Unaweza kujiuliza ni kwanini Liverpool na Man United wanachukiana hivi licha ya kutoka miji tofauti, basi majibu yapo hapa.

Bifu la Majiji

Sababu za kisoka ndiyo zimekuwa zikitajwa zaidi katika bifu la Liverpool na Man United, lakini kiuhalisia uadui kati ya klabu hizi zenye mafanikio zaidi England umeanzia nje ya soka.

Unaambia chuki ya Liverpool na Man United ilianzia katika Majiji yao ambayo yako Kaskazini Magharibi mwa England, huku tofauti kati ya Jiji la Liverpool na Manchester zikiwa ni kilomita 56.

Sababu za kiuchumi zilisababisha chuki kati ya majiji haya mawili enzi za Mapinduzi ya Viwanda mwanzo Jiji la Manchester lilikuwa maarufu sana, lakini kufika Karne ya 18, Jiji la Liverpool liliibuka na kuwa na bandari muhimu kwa ajili ya ukuaji wa viwanda vya pamba vya kaskazini mwa England.

Bandari hiyo ikalikuza sana Jiji la Liverpool na kulifunika Jiji la Manchester, uhusiano kati ya majiji hayo uliimarishwa na uanzishwaji wa kampuni ya usafirishaji ya Mersey & Irwell, ujenzi wa mfereji wa Bridgewater na reli ya kwanza duniani kati ya mji na mji Liverpool & Manchester Railway.

Lakini, ujenzi wa mfereji wa meli wa Manchester, uliotekelezwa na wafanyabiashara wa Manchester na kupingwa sana wanasiasa wa Jiji la Liverpool, ndiyo ulioanza kutibua mambo na hali kuwa mbaya.

Baada ya kumalizika kwa mfereji huo mwaka 1984, ukaibuka uadui kati ya mabahari wa Liverpool na wafanyakazi wa Manchester na hii ilikuwa ni miezi mitatu tu kabla ya mechi ya kwanza kati ya Liverpool dhidi ya Newton Heath (sasa Man United).

Japokuwa, kuna klabu nyingine kwenye miji hii lakini mafanikio ya Liverpool na Man United ndiyo sababu kubwa ya bifu la majiji kuhamia katika klabu hizi.

Mechi ya kwanza

Newton Heath (Man United kabla ya kubadili jina mwaka 1902) – iliburuza mkia kwenye msimamo wa Ligi Daraja la Kwanza msimu wa 1893-94, huku Liverpool ikishinda taji la Ligi Daraja la Pili bila kufungwa.

Hii ilimaanisha timu hizo zilitakiwa kukutana kusaka nani acheze Ligi Daraja la Kwanza msimu uliofuata. Liverpool ilishinda mechi hiyo kwa mabao 2-0 na kupanda daraja wakati Newton Heath ikishuka na hapo ndipo upinzani wa uwanjani ukazaliwa.

Mwanzoni miaka ya 1900

Liverpool ilishinda taji la kwanza la ligi mwaka 1901, wakaongeza la pili 1906, huu ulikuwa msimu ambao Man United ilirudi Ligi Daraja la Kwanza. Mwaka 1908 Man United ikatwaa taji lake la kwanza la ligi na kushinda Ngao ya Jamii ya kwanza kabisa huku mwaka mmoja baadaye wakitwaa Kombe la FA. Mwaka mmoja baadaye Man United ilishinda taji la Ligi na Ngao ya Jamii tena.

Ligi ikasimama kupisha Vita ya Kwanza ya Dunia, na kurudi 1919. Liverpool ikitwaa ubingwa 1922 na 1923, huku Man United ikipotea. United ilishuka tena 1923. Kisha klabu zote zikapitia ukame.

Mwaka 1940 na kuendelea

Man United ilianza kutulia katika mwaka 1945 baada ya Matt Busby kupewa timu. Kabla ya kufundisha United, Busby aliwahi kuchezea Manchester City na Liverpool. Alishawahi kuwa nahodha wa Liverpool.

Baada ya kustaafu soka Liverpool walimpa Busby nafasi ya kuwa kocha msaidizi, lakini akagoma kwa sababu aliamini ana vitu vingi anaweza kufanya, ila akiwa chini ya mtu hatafanikiwa.

Hivyo, baada ya Man United kumfuata na kumpa kazi kama kocha na kukubaliana na mahitaji yake akaamua kutua Old Trafford. Mwanzo alipewa mkataba wa miaka mitatu lakini akaishawishi klabu impe miaka mitano.

Utawala wa Busby

Japokuwa Busby hakufanikiwa haraka Man United, lakini alileta utulivu na kuanza kuijenga timu taratibu huku akitoa upinzani kwa Liverpool timu ambayo aliichezea kwa mafanikio.

Katika utawala wa Busby, Man United ikaanza kupanda wakati ambao Liverpool ilikuwa inapotea. Busby aliipa Man United ubingwa wa kwanza baada ya miaka 40 hii ilikuwa 1952. United ikatawala na kutwaa mataji la ligi 1952, 1956, 1957, 1965 na 1967: Kombe la FA 1963 na wakawa timu ya kwanza kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1968, yote haya yalifanywa na Busby, ambaye soka lake alicheza Liverpool, na hii iliwauma watu wa Anfield.

Liverpool yarudi kileleni

Mwanzoni mwa miaka ya 1960, Liverpool ilianzia kurudi kileleni chini ya Bill Shankly, aliwarudisha Ligi Daraja la Kwanza mwaka 1962. Na kuwapa ubingwa 1964, 1966, 1973 na Kombe la FA 1974 kisha akasepa.

Kati ya mwaka 1974 na 1991, Liverpool ilifundishwa na makocha watatu, Bob Paisley, Joe Fagan na Kenny Dalglish na wote walikuwa na mafanikio wakashinda mataji 11 ya ligi 1974, 1976, 1977, 1979, 1980, 1982, 1983, 1984, 1986, 1988 na 1990. Kombe la FA 1974, 1986 na 1989, Kombe la Ligi 1981, 1982, 1983 na 1984. Kombe la Ulaya 1977, 1978, 1981 na 1984. Super Cup ya Ulaya 1977, Kombe la UEFA 1973 na 1978.

Lakini baada ya kutwaa taji la Ligi mwaka 1990 mambo yakabadilika tena.

Ujio wa Sir Alex Ferguson

Baada ya kuanza vibaya maisha yake ya ukocha katika kikosi cha Man United, Ferguson alitulia na kuanza kuitoa Liverpool katika kilele cha mafanikio na kuhakikisha ubingwa wa Liverpool wa mwaka 1990 unakuwa wa mwisho kwao katika ligi hadi leo.

Ferguson alitua Man United 1986, lakini alitwaa taji lake la kwanza katika msimu wa 1989-90, baada ya kubeba Kombe la FA, Msimu uliofuata akabeba Kombe la Washindi Ulaya, msimu wa 1991-92 walibeba Kombe la Ligi na Uefa Super Cup.

Utawala wa Man United

Baada ya kumsajili Eric Cantona kutoka Leeds, katika msimu wa 1992/93 mambo yalibadilika, United ikatwaa ubingwa wao wa kwanza wa Ligi tangu mwaka 1967. Ubingwa huo ukafungua milango ya mafanikio Old Trafford.wakitwaa mataji 13 ya Ligi Kuu katika kipindi cha miaka 20 ya Fergie, Ligi ya Mabingwa mara mbili.

Katika kipindi hiki Liverpool hawakuwa na mafanikio makubwa sana, walitwaa Kombe la FA mara tatu, Kombe la Ligi mara nne, Kombe la UEFA mara moja na Ligi ya Mabingwa mara 1.

Hadi kufika mwaka 1990 Liverpool ilikuwa inaongoza kwa kuwa na mataji mengi ya Ligi 18, lakini chini ya Ferguson Man United ilitoka mataji saba hadi kuwakuta na kuwapita kufikisha mataji 20 na kuwa klabu inayoongoza kwa kuwa na mataji mengi ya Ligi Kuu.

Kushuka kwa Man United

Tangu Ferguson astaafu kufundisha soka mwaka 2013, Man United imepotea huku makocha David Moyes, Louis van Gaal na Jose Mourinho wakishinda kuendeleza ubabe wake. Liverpool imekuwa bora sana chini ya Jurgen Klopp na msimu huu inaandika rekodi kila kukicha imetwaa taji la Ligi ya Mabingwa msimu uliopita na kufikisha mataji sita ya Ulaya na sasa inatafuta taji la Ligi Kuu kwa mara ya kwanza tangu 1990.

Chuki SASA

Historia kati ya timu hizi imezaa chuki kati yao na siku zote hakuna mechi ndogo kati Man United na Liverpool kwao kila mechi ni fainali.

Ule usemi wa adui muombee njaa unathibitishwa na uadui kati ya klabu, unaambiwa mashabiki wa Man United wana wimbo wao ambao hutumika kuwadhihaki Liverpool kuhusiana na majanga ya Hillsborough na Heysel yaliyoua mashabiki wengi wa Majogoo wa Anfield.

Lakini, mashabiki wa Liverpool nao wana wimbo wa kuwadhihaki Man United kuhusiana na ajali ya ndege ya jijini Munich iliyoua wachezaji kadhaa wa kikosi cha kwanza cha miamba hiyo.

Kuna mechi Gary Neville alipigwa faini kwa kushangilia goli mbele ya mashabiki wa Liverpool, wakati Steven Gerrard aliwahi kunukuliwa akisema kuwa, hajawahi kubadilishana jezi na mchezaji wa Man United kwa sababu anaichukia klabu hiyo na hawezi kuwa na jezi yake.

Hawauziani wachezaji

Kuna wachezaji wamewahi kucheza klabu zote mbili, lakini ili hilo lifanikiwe ni lazima kwanza uzunguke. Mara ya mwisho kuuziana mchezaji ilikuwa mwaka 1964, wakati Phil Chisnall alipotoka Man United na kutua Liverpool. Lakini, tangu wakati huu timu hizi zimegoma kuuziana wachezaji.

Mwaka 2007, Liverpool walitaka kumsajili Gabriel Heinze kutoka Man United, Ferguson akagoma huku akiweka wazi kuwa ni bora Heinze asugue benchi kuliko kumuuza Liverpool kwa sababu huo ni mwiko, lakini mwisho wakamuuza kwenda Real Madrid na kuitosa Liver.