Okwi asubiriwa kuosha nyota Shinyanga

Wednesday February 14 2018

 

By SADDAM SADICK,

Wakati Simba ikitarajia kujitupa uwanjani leo kuwavaa Mwadui FC kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu, macho na masikio ya wadau wa soka yatakuwa kwa nyota wao, Emanuel Okwi kama ataendelea kuandamwa na mzimu wa kutofunga mabao kwenye viwanja vya ugenini.

Okwi ambaye anaongoza kwa idadi ya mabao (13) tangu Ligi Kuu ianze hajawahi kufunga nje ya uwanja wa Taifa na kesho Alhamisi macho na masikio ya wadau wa soka yatakuwa kwake kuona kama atavunja mwiko.

Tangu kuanza kwa mzunguko wa pili Simba ndio mechi yao ya kwanza kutoka nje ya Dar es Salaam, kwani mchezo ambao ungeitoa uwanja wa Taifa dhidi ya Ruvu Shooting ulipigwa kwenye uwanja huo na kushinda mabao 3-0, kisha kuwalaza Azam bao 1-0.

Hata juzi wakati Simba ikiwa dimba la Taifa ikipambana na Gendarmarie kwenye mchezo wao wa kombe la Shirikisho,Mshambuliaji huyo aliipachikia bao timu yake dakika za mwisho na kufanya mpambano kuisha kwa ushindi wa mabao 4-0.

Mdau wa soka na mchezaji wa zamani zamani wa Simba,Mbui Yondani alisema kuwa kutokana na uchangamfu uliopo kwa sasa kikosini humo, lazima Okwi afunge.

“Kwa sasa siwezi kuamini kwamba Okwi atashindwa kufunga ugenini,nina uhakika atawafunga tena mapema sana,nyie subirini mtaona kabla ya dakika 90,” alisema Straika huyo mkongwe.

Mchezaji wa zamani wa Pamba,Salmin Kamau alisema kuwa Straika huyo kama atapata nafasi uwezekano wa kufunga anao na kwamba mara kadhaa viwanja vya ugenini vimekuwa vinampa shida.

“Kesho (leo) anaweza kufunga kama atapata nafasi,unajua ugenini wachezaji wanakamia sana,lakini hata ubovu wa viwanja unachangia,” alisema Kamau.

Simba itawavaa Mwadui ikiwa kileleni mwa msimamo baada ya kuvuna pointi 41,Yanga wakiwa nafasi ya pili kwa pointi 34,huku ijivunia pia kutopoteza mchezo wowote na kufunga mabao mengi (39) hadi sasa.

 

Advertisement