Ole karibu Manchester

Manchester,England. KARIBU jijini Manchester Ole. Ndio leo Jumatano kocha wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer atakuwa anakaribishwa rasmi kwenye soka la wababe wa jiji hili.

Wakati chama lake likiwa na majanga ya kucheza soka la ovyo na kufungwa mechi sita kati ya nane, Ole anakutana kwenye mtanange wa kukata na shoka kwa kuwakaribisha mahasimu wao, Manchester City ya Pep Guardiola.

Ugumu wa mchezo huo ambao ndio utakuwa wa kwanza kwa Ole tangu amekabidhiwa mikoba ya Jose Mourinho, ni kuwa Man City wanataka kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kubeba ubingwa huku United ikijaribu kusaka nafasi kuona kama inaweza kupambana kumaliza ndani ya Top Four msimu huu ili ifuzu Ligi ya Mabingwa.

Tayari Ole amekutana na mechi ngumu tangu akabidhiwe mikoba hiyo, lakini ndio Manchester Derby yake ya kwanza kama kocha wa mashetani wekundu wa Old Trafford. Joto na ugumu wa mechi hizi Ole analifahamu sana, lakini tofauti na siku zingine leo atasimama kwenye benchi akiwa kocha na sio mchezaji kama alivyokuwa zamani wakati Man United ikiwa chini ya Sir Alex Ferguson.

Pia, Ole atawaongoza vijana wake kwenye dimba la Old Trafford kusaka ushindi kujaribu kurejesha heshima na kulipa kisasi kwani, kwenye mechi ya kwanza Man United ikiwa chini ya Mourinho ilichapwa mabao 3-1 pale Etihad. Hata hivyo, wakati joto la mchezo huo likizidi kupanda kuna hatari kubwa matokeo mabaya kwa Man United yakaongeza vuruguvu la mabadiliko ndani ya kikosi hicho. Kwa sasa kuna taarifa kwamba, mastaa wake kadhaa wanaweza kuomba kuondoka kama timu itashindwa kufuzu katika Ligi ya Mabingwa Ulaya. Tishio hilo linaongeza ugumu wa mchezo huo kwani, licha ya Man United kupoteza mechi nyingi lakini itataka kuamsha matumaini ili kupata nafasi ya kushiriki michuano hiyo mikubwa ngazi ya klabu barani Ulaya msimu ujao.

Habari kutoka ndani ya Old Trafford zinaeleza kwamba, kipa namba moja na tegemeo ndani ya kikosi hicho, David De Gea, kiungo Paul Pogba na straika mwenye miraba minne, Romelu Lukaku wanafikiria kuondoka kama chama hilo halitakuwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kwa sasa Manchester United iko nafasi ya sita kwenye msimamo ikiwa na pointi zake 64 ilizovuna kwenye mechi 34.

Baada ya kukipiga na Man City, itasaliwa na mechi tatu dhidi ya Chelsea (Old Trafford), Huddersfield Town (ugenini) kisha itamaliza na Cardiff City uwanjani Old Trafford. Kwa upande wake Manchester City ambayo inachuana na Liverpool kwenye mbio za ubingwa msimu huu, itaingia kwa lengo moja la kupata alama tatu ambazo zitaifanya kukaa juu ya msimamo ikiweka pengo la alama mbili zaidi. Hata hivyo, kwenye mchezo huo Guardiola ataingia uwanjani bila mtengeneza mipango wake, Kevin De Bruyne ambaye atazikosa mechi zote za ligi zilizobaki baada ya kuumia kwenye mchezo dhidi ya Tottenham. Mechi nyingine ambayo itapigwa leo usiku ni kwa Wolves kuwaikaribisha Arsenal kwenye dimba la Molineux Stadium ambalo ni kama machinjioni kwa wababe wengi msimu huu. Arsenal ya Unai Emery ambayo inawania nafasi ya kumaliza Top Four kama ilivyo kwa Man United, itaingia kwenye mchezo huo ikitoka kuchapwa katika uwanja wake wa nyumbani wa Emirates na Cryastal Palace kwa mabao 3-2.