Gabon wataka ukweli afya ya Bongo

Friday November 9 2018

 

Libreville, Gabon. Maofisa wa ngazi ya juu katika chama tawala cha Gabon, wametoa wito kwa Serikali kuweka wazi hali ya afya ya Rais Ali Bongo, ambaye amelazwa nchini Saudi Arabia huku uvumi ukisema amepooza.
Kamati ya ushauri ya chama cha Gabonese Democratic Party (PDG) imesema ufafanuzi ni lazima utolewe ili "kuihakikishia jamhuri" wakati huu "upepo wa uvumi katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii."
Wakati ikisisitiza kwamba suala la “kuhamisha mamlaka si ajenda ya mjadala” kamati hiyo ilionya kwamba kukosekana kwa habari sahihi “kunaweza kuchochea chuki, migawanyiko na kudhoofisha hali ya siasa”.
Bongo, 59, aliugua Oktoba 24 alipokuwa ziarani Riyadh, Saudi Arabia kuhudhuria mkutano wa jukwaa la kiuchumi.
Msemaji wa Serikali Ike Ngouoni alisema madaktari walimpima na kugundua kuwa “alikuwa akisumbuliwa na uchovu” na wakamtaka apate mapumziko.
Lakini chanzo kimoja cha nje ambacho kipo karibu na familia kiliiambia AFP Jumatano kuwa Bongo amepata kiharusi.
Kukosekana kwa habari rasmi pamoja na kumbukumbu za usiri wa kifo cha baba yake Bongo, Omar Bongo, ambaye alifia ofisini mwaka 2009 baada ya kutawala miongo kadhaa – kumesababisha uvumi kutawala.

Advertisement