Pawasa, Costa wampa neno Mbelgiji Simba

Dar es Salaam.Wakati Juuko Murshid akitajwa kuziba pengo la Erasto Nyoni katika kikosi cha Simba kitakachoivaa JS Saoura ya Algeria, Kocha Patrick Aussems, amepewa mbinu ya kumtumia ili amudu vyema mchezo huo wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba itacheza na JS Saoura Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na beki huyo raia wa Uganda amepewa jukumu la kucheza pacha na Paschal Wawa katika nafasi ya ulinzi.

Licha ya kuwa na idadi kubwa ya mabeki wa kati, Aussems amemteua Juuko kuziba pengo la Nyoni aliyeumia goti katika mchezo wa Kombe la Mapinduzi dhidi ya KMKM.

Juuko anabebwa na rekodi nzuri katika mechi za timu ya Taifa ya Uganda, ‘The Cranes’ ambako amekuwa beki tegemeo wa kikosi cha kwanza kulinganisha na Simba anakopata nafasi mara chache.

Beki huyo alijiunga na Simba akitokea Victoria University mwaka 2014 na alianza kucheza timu ya Taifa Novemba 12, 2015 katika mechi za kufuzu Kombe la Dunia nchini Russia dhidi ya Togo ambako aliwadhibiti washambuliaji nyota Ayite Jonathan aliyekuwa akicheza soka Uturuki na Dossevi Mathieu aliyekuwa Olympiakos Pirates.

Pia alicheza mechi zote za Kundi E lililokuwa na vigogo Misri, DR Congo na Ghana zilizoundwa na idadi kubwa ya wachezaji waliokuwa wakicheza soka la kulipwa nje ya Afrika.

Baadhi ya nyota aliopambana nao katika mechi hizo ni Asamoah Gyan aliyekuwa akicheza Shanghai SIPG ya China na Jordan Ayew aliyekuwa Aston Villa ya England.

Beki huyo wa kati alijenga jina baada ya kumdhibiti mshambuliaji nyota wa Liverpool, Mohamed Salah, katika mchezo wa Agosti 31.

Mbali na rekodi hiyo, mwaka jana, Juuko amecheza mechi ngumu dhidi ya Cape Verde, Lesotho na Tanzania na kuipa Uganda tiketi ya kufuzu Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) ambako fainali zitachezwa Cameroon.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, baadhi ya mabeki wa kati waliowahi kucheza Simba na Taifa Stars, walisema Juuko ni beki hodari, lakini anapaswa kuandaliwa kisaikolojia kuziba pengo la Nyoni.

Kocha wa timu ya Taifa ya ufukweni, Boniface Pawasa alisema anashangazwa Juuko kukosekana katika kikosi cha kwanza cha Simba.“Juuko anacheza kwa kiwango bora anapokuwa na timu yake ya Taifa, sijui kwanini Simba haaminiwi,”alisema Pawasa.

Alisema ingawa hafahamu mfumo wa Aussems katika mchezo wa Jumamosi, lakini endapo atamuanzisha Juuko, anaamini atacheza kwa ufanisi.

“Ni mchezaji anayetumia nguvu, huenda hilo ndilo linampa woga kocha akidhani anaweza kusababisha faulo nyingi, lakini ni wakati wa kumuandaa na kumjenga kisaikolojia.

“Kocha asimfanye Juuko kuwa mbadala baada ya kuumia Nyoni ndipo afikirie kumunzisha, hapana, yule ni miongoni mwa mabeki bora kilichopo ni kumjengea hali ya kujiamini, naamini kama akimuaminisha atabaki katika kikosi cha kwanza,”alisema Pawasa.

Naye Victor Costa alisema Juuko anatakiwa kupewa ushauri wa kitaalamu ili kumjengea uwezo wa kucheza vyema mchezo huo kwa kuwa ni mchezaji hodari. “Juuko ni beki mzuri ingawa pale Simba hapati nafasi ya kuanza, kama ataaminiwa na kuandaliwa kisaikolojia, mashabiki wa Simba watamsahau Nyoni,”alisema Costa.

Kocha wa Biashara United Amri Said alisema Juuko ni hodari ana kasi, anacheza mipira ya juu, hivyo ana sifa za kucheza pacha na Wawa.

“Sina wasiwasi naye kwenye mechi za kimataifa, amecheza The Cranes mechi tafu kuliko hiyo ambayo Simba inakwenda kucheza Jumamosi,”alisema Amri.