Picha la Mahrez limeisha atua Man City

Wednesday July 11 2018

 

Manchester, England. Hatimaye klabu ya Manchester City imefanikiwa kumaliza mvutano wa muda mrefu kwa kufanikiwa kumsajili winga wa Leicester City, Riyad Mahrez, raia wa Algeria.

City wamevunja rekodi yao ya usajili kwa kulipa Pauni 60 milioni kwa mchezaji huyo mwenye miaka 27, ambaye amesaini mkataba wa miaka mitano, akiwa mchezaji wa kwanza kusajiliwa na timu hiyo katika dirisha hili la usajili.

Mabingwa hao wa Ligi Kuu England, walijiondoa katika mbio za kumuwania Mahrez, Januari mwaka huu baada ya Leicester kumzuia kuondoka, licha ya awali kumruhusu azungumze na City na kufikia makubaliano.

Msimu uliopita Mahrez aling’ara sana na anaondoka klabuni hapo akiwa na rekodi bora ya ufungaji baada ya kufunga mabao 48 katika michezo 179 aliyocheza huku 39 yakiwa ya Ligi Kuu England.

“Nafurahi nimejiunga na City, nafikiri nitapiga hatua sasa, bila shaka tutafanikiwa zaidi misimu ijayo, nadhani aina yangu ya uchezaji inaweza kuwa nzuri zaidi chini ya Kocha Pep Guardiola,” alisema mchezaji huyo baada ya kusaini.

Mahrez alichaguliwa kuwa mchezaji bora wa mwaka baada ya Leicester kuwashangaza wengi kwa kuwa mabingwa wa England msimu wa 2015-16.

Leicester imemfagilia mchezaji huyo na kumtakia mafanikio huko aendako ikisema alicheza kwa moyo mmoja akiwa karibu na mashabiki wao kwa miaka minne na nusu ndani ya klabu.

Mahrez aliomba kuihama Leicester, Januari mwaka huu lakini ikashindikana baada ya Manchester City kukataa kutoa Pauni 95 milioni iliyokua ikihitajika na klabu yake.

Advertisement