Pochettino ampa masharti Woodward kutua Man United

Sunday January 19 2020

 

LONDON, ENGLAND. MAURICIO Pochettino ameripotiwa amempa masharti Ed Woodward kama anamhitaji aende kuwa kocha mpya wa Manchester United.

Kocha huyo Muargentina, Pochettino aliyefutwa kazi huko Tottenham Hotspur amemwambia Woodward kama anataka aende kuwa kocha wa Man United basi ahakikishe apewa nguvu kubwa ikiwamo uamuzi wa wachezaji wa kuwasajili.

Pochettino amekuwa akipewa nafasi kubwa ya kwenda kuchukua mikoba ya kuinoa klabu hiyo ya Old Trafford.

Kwa sasa Man United ipo chini ya Ole Gunnar Solskjaer, lakini haitashangaza kama atafunguliwa milango ya kutokea kama atashindwa kuisaidia timu kufuzu kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Pochettino ameripotiwa yupo tayari kuchukua mikoba hiyo, lakini kama tu masharti yake yatafuatwa. Pochettino anamtaka Woodward asiwe na kauli ya mwisho kwenye suala la usajili kutokana na kuwa na rekodi ya kufanya dili za hovyo miaka ya karibuni.

Mwaandishi wa TalkSPORT, Phil Brown alisema: “Nilichoambiwa ni kwamba Man United wamekuwa wakizungumza na Pochettino kwa wiki kadhaa sasa. Hataki kazi ya kuinoa timu hiyo kwa sasa hadi mwisho wa msimu. Lakini, hataki pia kama masharti yake hayatazingatiwa.

Advertisement

“Hivi vitu viliambiwa na mtu maarufu, ambaye nimekuwa nikimwaamini kwa asilimia 100. Ameniambia dili la Pochettino kwenda Man United haliwezi kutokea kwa sasa hadi mwisho wa msimu. Pochettino hana wakala na Ed Woodward si mtu anaweza kuonekana tu hadharani hovyo.”

Advertisement