Rage: Mechi ya Waarabu ilifaa Saa 8:00

Muktasari:

  • Simba na Al Ahly zitapambana keshokutwa kwenye mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia saa 10:00 jioni.

Dar es Salaam. Miamba ya soka Misri Al Ahly ilitarajiwa kuwasili nchini saa 9 usiku wa manane kuamkia leo wakitokea Cairo, Misri tayari kwa mchezo dhidi ya Simba utakaochezwa keshokutwa kuanzia saa 10:00 jioni kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam lakini Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Ismail Aden Rage amesema ilifaa wachezeshwe saa 8:00 jua kali.

Wachezaji wa Al Ahly wakiongozwa na kocha wao raia wa Uruguay, Lassarti waliondoka jana usiku saa 4:30 na walitarajiwa kufika saa 10:00 alfajiri tayari kwa mchezo huo.

Al Ahly ndio inayoongoza kundio hilo la D ikiwa na pointi saba ikifuatiwa na AS Vita na Simba na JSS zinafuatia.

Endapo Simba itaing’ang’ania timu hiyo, itafikisha pointi sita na kushika nafasi ya pili, lakini pia itategemea matokeo ya mechi ya marudiano ya JSS na AS Vita kule Algeria.Simba ilifungwa mabao 5-0 wakati timu hizo zilitoka sare ya 2-2 mjini Kinshasa.

Akizungumza na Mwananchi, Rage alisema kuwa mbinu moja wapo ya kuwachosha Waarabu ilikuwa kuwachezesha mchana wa jua kali.

“Kule kwao hali ya hewa ni baridi sana na usiku ndio kuna baridi kali, na ndio maana wakawapeleka Simba kwenye baridi, inawezekana na ndicho kiliwashinda kucheza kutokana na hewa kuwa nzito, sasa ili kuwachosha na joto, mechi ingepigwa saa 8 au 9 kwenye jua kali,” alisema Rage.

Rage aliyewahi kuongoza Simba aliwataka wachezaji wa timu hiyo kujituma na kusimama kila mmoja na mtu wake bila kuwapa nafasi. “Simba wanajiachia mno, inatakiwa kuwabana na kutowapa nafasi, kila mmoja acheze na mtu wake ili kuwabana,” alisema Rage.

Akizungumzia mchezo huo, nahodha msaidizi wa timu hiyo na beki wa pembeni wa Simba, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ alisema watakomaa kuhakikisha wanavuna pointi zote tatu dhidi ya Al Ahly ya Misri ingawa amekiri kazi itakuwepo.

Tshabakaka alisema wameendelea kufanyia kazi upungufu katika kikosi chao ikiwemo safu ya ulinzi na naamini katika mchezo huo hawataruhusu bao.

“Kila mara tumeendelea kuimarika na kupunguza makosa na ndio maana hata kwenye mchezo wa Mwadui hatukuruhusu bao hivyo tutapambana mchezo dhidi ya Al Ahly tufanye hivyo hivyo.

Utakuwa mchezo mgumu kwani wapinzani wetu ni moja ya timu kubwa na bora Afrika hivyo haitakuwa kazi rahisi kuwafunga lakini tuko nyumbani na mcheza kwao hutunzwa hivyo naamini hiyo mechi tunashinda”alisema Tshabalala.

Tshabalala amewataka mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi siku hiyo na kujaza uwanjani kwani uwepo wao utawapa nguvu ya kupambana zaidi.

Tunashukuru mashabiki wetu wamekuwa wakitusapoti katika hali zote iwe tumeshinda au tumepoteza hivyo nawaomba waendelee kutuunga mkono kwa kujaa uwanjani na kutupa sapoti na sisi hatutawaangusha,” alisema.