Raptors yatinga fainali NBA Kanda ya Magharibi

Muktasari:

Timu nyingine zilizotinga fainali hizo za Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani ni Milwaukee Bucks, Golden State Worriors na Portland Trail Blazers


Kawhi Leonard Jumapili usiku alifunga katika sekunde ya mwisho wakati Toronto Raptors ilipofuzu kucheza fainali za Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Marekani (NBA), Kanda ya Mashariki kwa kuibuka na ushindi wa pointi 92-90 dhidi ya Philadelphia 76ers katika mchezo mkali wa saba wa nusu fainali za Kanda ya Mashariki.
Mechi hiyo ambayo mshindi ndio angekata tiketi hiyo ya kusonga mbele ilikuwa kali, yenye ushindani katika fainali hizo zisizotabirika baada ya kila timu kufanya juhudi kubwa kabla ya Leonard kumaliza ubishi.
"Nilipata mpira uliopotea na uliokuwa na matunda," alisema Leonard akizungumzia mechi hiyo ni ya kwanza katika historia ya NBA kwa mshindi kuamuliwa na mpira uliorushwa wakati filimbi ya mwisho ikiwa imeshapulizwa katika mchezo wa saba wa fainali za kanda.
"Nilirushwa kwa nguvu kadri nilivyoweza. Niliushika vizuri juu na kuufanya mpira udunde kilaini na kuishia kutumbukia kwenye goli."
Raptors imesonga mbele kwenye fainali ya nne ya NBA ambako itakumbana na Milwaukee Bucks, inayopewa nafasi kubwa katika mechi ya kwanza itakayofanyika Jumatano.
Huku ubao ukisomeka pointi 90-90 na mchezo ukionekana kuelekea katika muda wa nyongeza, Leonard aliamua kujibebesha mzigo wote mwenyewe. Alikimbia mbele ya goli na kwenda upande wa kulia wa uwanja na baadaye kurusha golini mpira.
Wakati mpira ulipodunda juu ya duara mara mbili, Leonard alichuchumaa kusubiria utumbukie na muda mfupi baadaye alikuwa amezingirwa na mashabiki wanaoshangilia ushindi baada ya mpira kutumbukia golini.
Leonard alimaliza mechi hiyo akiwa amefunga pointi 41 huku Pascal Siakam akifunga pointi 11 na kunyakua ribaundi 11 kwa upande wa Raptors, ambayo inategemea kufika fainali kwa mara ya kwanza katika historia yao ya kushiriki NBA.
Katika mechi nyingine ya fainali za kanda, CJ McCollum aliongoza ushindi wakati Portland Trail Blazers iliposhinda mchezo wa saba dhidi ya Denver Nuggets kwa pointi 100-96.
Portland ilitegemea uwezo wa McCollum aliyefunga pointi 37 na kuiondoa Nuggets mjini Denver na kukata tiketi ya kucheza fainali za Kanda ya Magharibi dhidi ya mabingwa wa NBA, Golden State.