Ratiba Ligi Kuu, CAF zaivuruga Simba SC

Dar es Salaam. Wakati Simba leo ikicheza mechi yake ya kiporo dhidi ya Ruvu Shooting, klabu hiyo imesema ugumu wa ratiba unaiweka katika mazingira magumu ya kujiandaa kwa mchezo ujao wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Simba imefuzu robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya kuilaza AS Vita ya DR Congo mabao 2-1, katika mchezo uliochezwa Jumamosi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crecentius Magori, alisema ingawa wanasubiri droo ya mechi za robo fainali, lakini ugumu wa ratiba ya Ligi Kuu ni changamoto kubwa kwa upande wao.

“Kitendo cha kuingia robo fainali, maana yake viporo vyetu vya Ligi Kuu vitaongezeka zaidi, mzigo mkubwa utakuwa mbeleni kuvicheza,” alisema Magori.

Mtendaji huyo alidai wanasubiri droo ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) ambako kuna uwezekano mechi ya kwanza itachezwa Aprili 6 nyumbani au ugenini na maruadiano Aprili 12.

“Siku ambazo tunaweza kucheza mashindano ya kimataifa, ratiba ya ligi inaonyesha tutakuwa na mechi Aprili 3, 6, 9 na 12, ikiwa hivyo maana yake hakuna namna Bodi ya Ligi inabidi kutufikiria ili tupate muda wa kujiandaa pia, maana yake ni nini… viporo vyetu vitaongezeka.

Ratiba ya mechi zijazo za Simba inaonyesha kati ya Aprili 3 itacheza na JKT Tanzania kabla ya kuivaa Aprili 6 na KMC.

“Changamoto hiyo ni kwenye robo fainali, endapo tutafuzu nusu fainali na hata fainali ambayo ndiyo mipango yetu bado ratiba itakuwa ngumu kwetu, kwani lazima Ligi iishe Mei.

Magori alisema kwa namna ilivyo benchi la ufundi litalazimika kutumia wachezaji wote waliosajiliwa na Simba kucheza kwa manufaa ya ustawi wa klabu.

“Hilo ni jukumu la mwalimu na bahati nzuri analitambua, ili kupunguza changamoto ya wachezaji kuchoka kucheza mfululizo lazima wazunguke,” alisema Magori.

Tamko Bodi ya Ligi

Pamoja na dhamira ya Simba kuomba baadhi ya mechi zake zisogezwe mbele, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema timu hiyo inapaswa kujiandaa kwa mechi zote za Ligi Kuu na CAF.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Wambura alisema kuwa hakutakuwa na muda wa kujiandaa, hivyo Simba inatakiwa kujiandaa kwa zake zote za mashindano.

“Watacheza kulingana na kanuni inavyosema kila baada ya saa 72 wanacheza mechi, hakuna muda wa kujiandaa cha msingi ni kufuata kanuni tu,” alisema Wambura.

Kauli ya Mkwasa, Kipingu

Wakati Simba ikidai changamoto ya ratiba inaweza kuwa kikwazo kwao, aliyewahi kuwa Kocha wa Yanga na Taifa Stars, Charles Mkwasa alisema wachezaji njia bora ya kuinusuru timu hiyo ni kuwaandaa wachezaji wake kisaikolojia.

Mkwasa alisema wachezaji wanapaswa kujengwa kimwili na kiakili kwa lengo la kuwaweka sawa kukabiliana na ratiba ngumu, vinginevyo wanaweza kuwatoa mchezoni kabla ya mashindano.

“Nakumbuka imewahi kutokea nikiwa kocha wa Yanga, tulicheza mechi nne ndani ya wiki moja, wachezaji walichoka, hata kwa Simba inaweza kuwafanya wachezaji kupoteza mwelekeo,” alisema Mkwasa.

Mwenyekiti wa zamani wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Kanali Mstaafu Idd Kipingu alisema kucheza mfululizo kwa timu kunaweza kusababisha idadi kubwa ya majeruhi.

“Mechi mfululizo zinaweza kutengeneza majeruhi wengi, wachezaji waandaliwe kisaikolojia ili kukabiliana na mazingira hayo,” alisema Kipingu.

Droo ya robo fainali itafanyika kesho mjini Cairo, Misri na Simba inatarajiwa kupangwa dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, Wydad Casablanca ya Morocco au Esperance ya Tunisia zilizoongoza katika makundi yao.

Timu nyingine zilizofuzu robo fainali ni Mamelodi Sundown (Afrika Kusini), Horoya (Guinea), Al Ahly (Misri) na CS Costantine ya Algeria.