Ratiba yaongeza presha Ligi Kuu

Sunday May 26 2019

 

By Charles Abel, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati kipigo cha mabao 2-0 ambacho Kagera Sugar imekipata kutoka kwa JKT Tanzania jana asubuhi kikiinusuru rasmi Singida United iliyokwepa kushuka daraja, ratiba mechi za mwisho za ligi hiyo inaongeza presha kwa timu sita ambazo kila moja inalazimika kushinda ili ijihakikishie kubaki.

Matokeo ya mechi ya JKT dhidi ya Kagera Sugar jana, yanaifanya Singida United isiwe na uwezekano wa kushuka daraja hata kucheza mechi ya mchujo ikiwa itapoteza mchezo wake wa mwisho dhidi ya Coastal Union, kwani timu za Ruvu Shooting, Kagera Sugar, Mbao, Mwadui, Stand United na JKT Tanzania tatu kati yao haziwezi kuipiku kwa pointi kutokana na matokeo ambayo zitayapata kwenye mechi zao za mwisho.

Kitendo cha baadhi ya timu hizo kukutana zenyewe kwa zenyewe, kinafanya Singida iwe salama, kwani kwa sasa imezizidi pointi na matokeo yoyote kwenye mechi baina yao hayatokuwa na athari kwa timu hiyo kutoka mkoani Singida yenye pointi 45.

Ukiondoa Singida United, Alliance na Coastal Union ambazo zimejihakikishia kubaki kwenye ligi baada ya kupata ushindi kwenye mechi zao za raundi ya 37, hofu inahamia kwa timu sita ambazo ni Ruvu Shooting, Kagera Sugar, Mbao, Mwadui, Stand United na JKT Tanzania ambazo zitapaswa kuchanga vyema karata zao kwenye mechi za mwisho ili ziepuke ama kushuka daraja moja kwa moja au kucheza mechi za mchujo.

Mchezo baina ya Mbao FC watakaokuwa wenyeji dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa CCM Kirumba Mwanza, unatarajiwa kuwa na ushindani wa hali ya juu kwani timu hizo zimepishana pointi moja tu na mshindi atajihakikishia kubaki huku timu itakayofungwa ikijiweka kwenye hatari ya kushuka au kucheza mchujo kulingana na matokeo ya michezo mingine.

Ikumbukwe kuwa Mbao FC ipo nafasi ya 14 ikiwa na pointi 44 wakati Kagera Sugar yenye pointi 43 iko nafasi ya 17 ambayo ikiwa watamaliza hapo watatakiwa kucheza mchujo dhidi ya timu kutoka Ligi Daraja la Kwanza.

Advertisement

Mwadui FC iliyopo nafasi ya 19, inaweza kushuka rasmi ikiwa itafungwa dhidi ya Ndanda FC kwenye mechi ya mwisho nyumbani, lakini kama itashinda itafikisha pointi 44 na inaweza kubaki ikiwa tu JKT Tanzania, Mbao FC, Ruvu Shooting, Kagera Sugar au Prisons zitapoteza mechi zao.

Namna pekee ambayo itainusuru Ruvu Shooting kubaki Ligi Kuu msimu huu ni kupata ushindi dhidi ya Alliance nyumbani kwenye mechi ya mwisho na kisha kuombea wapinzani wake wengine wapoteze, vinginevyo sare au kipigo ama kitawashusha au kitawapeleka kucheza mechi za mchujo.

Prisons yenyewe itakuwa nyumbani kuwakaribisha Lipuli FC ikilazimika kushinda, vinginevyo kama itapoteza itajiweka kwenye uwezekano wa kushuka lakini kubwa zaidi wanaonekana watacheza mchujo ikiwa watapata matokeo tofauti na ushindi.

Akizungumzia nafasi ya timu yake kwenye Ligi Kuu, kocha wa JKT Tanzania, Mohammed Abdallah ‘Bares’ alisema faida ya kucheza nyumbani na maandalizi mazuri yatawabeba kwenye mechi ya mwisho na kubakia kwenye ligi.

Beki wa Prisons, Salum Kimenya alisema mechi yao ya mwisho ni ya kufa au kupona na watapambana kuhakikisha wanapata ushindi.

Advertisement