Real Madrid wataka Pauni 623 milioni kwa Isco

Muktasari:

  • Klabu ya Real Madrid ambayo ilikubali kumuuza mshambuliaji wake Cristiano Ronaldo Julai mwaka huu kwenda Juventus ni kama imestuka baada ya klabu hiyo kutaka kumsajili pia kiungo Isco, ambapo wamepandisha dau na kusema atauzwa iwapo tu Kibibi Kizee cha Turin kitakuwa tayari kutoa Pauni 623 milioni.  

Madrid, Hispania. Klabu ya Real Madrid imesema itakuwa tayari kumruhusu kiungo wake Isco ajiunge na timu yoyote anayoitaka iwapo italipwa Pauni 623 milioni.

Real imetangaza dau hilo kubwa baada ya kuona Juventus imejitokeza kutaka kumsajili kiungo huyo wa kimataifa wa Hispania, ikiwa ni miezi mitano tangu imng’oe Cristiano Ronaldo ambaye pengo lake linaitesa timu hiyo hadi sasa.

Klabu ya Real imeweka katika tovuti yake kwamba Isco ataruhusiwa kuondoka na kujiunga na Juventus ikiwa timu hiyo itakuwa tayari kulipa Pauni 623 milioni za kuvunja mkataba na ada ya uhamisho.

Ilisema licha ya kwamba Isco ana malalamiko yake kutokana na kutopangwa kila mara katika kikosi cha kwanza lakini bado yupo kwenye mipango ya kocha na Klabu kwa ujumla.

Mchezaji huyo mwenye miaka 26 amekuwa ahafurahii kuwekwa benchi na inaaminika ndiye aliyeomba kusajiliwa na Juventus.

Kocha mpya wa Real, Santiago Solari, hivi karibuni alidaiwa kutoa maneno yaliyomuudhi Isco kwa kumwambia anapaswa kufanya mazoezi zaidi kwa kuwa amejiachia na kuongezeko uzito.

Akijibu kauli hiyo ya kocha wake mchezaji huyo wa zamani wa Malaga jana Jumapili alitupia picha yake na kuuliza hivi nimekuwa mnene sana?, ikionyesha kuwa alikuwa akimjibu kocha wake huyo.

 Isco ambaye chini ya Solari amecheza dakika 88 pekee timu hiyo ikicheza michezo saba tangu kufukuzwa kwa kocha Julen Lopetegui, mbali ya Juventus anatakiwa na timu za Arsenal, Tottenham na Chelsea.