Rita yamkana Kilomoni Simba

Dar es Salaam. Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), imesema haina taarifa za Hamisi Kilomoni kuwa mdhamini wa klabu ya Simba.

Pia, imesema hakuna rekodi inayoonyesha Kilomoni, aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Klabu ya Simba bado yuko kwenye nafasi hiyo.

Akizungumza na gazeti hili jana, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Rita, Josephat Kimaro alisema taarifa za Simba zinawatambua wadhamini wanne, lakini Kilomoni sio miongoni mwao.

“Rekodi zetu tangu Novemba 2017 zinaonyesha wadhamini wa Simba ni Ramesh Patel, Abdul Abbas, Idd Mgoyi na Juma Kapuya,” alisema Kimaro.

Katika mtandao wa Rita unasema kipengele cha mabadiliko ya chombo, jina au marekebisho ya mdhamini lazima kuwakilisha nakala iliyothibitishwa na kumbukumbu ya mkutano uliothibitishwa ambao ulifanya mabadiliko ya jina na kurejesha cheti halisi cha zamani.

Akizungumzia barua ambayo ilionyeshwa juzi na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, Kimaro alisema ni halali kutoka Rita.

“Ni kweli ile barua ni yetu na kwenye kumbukumbu zetu huku Rita - Patel, Abbas, Kapuya na Mgoyi ndiyo wadhamini wa Simba, sifahamu kumbukumbu za nyuma zilikuwa vipi ila kuanzia Novemba 2017 hao niliowataja ndiyo wanasomeka kwetu kama wadhamini wa klabu ya Simba.”

Alisema tangu Novemba 2017 Rita haijapata malalamiko ya mtu au watu kupinga mabadiliko ya wadhamini. Kilomoni alipoulizwa kuhusu Rita kutomtambua kuwa miongoni mwa wadhamini wa Simba, alisema atatoa ufafanuzi wa suala hilo Jumatatu wiki ijayo.