Ronaldo, Guardiola wachangia mabilioni vita ya corona

Wednesday March 25 2020

 

By Mwandishi Wetu/AFP

Wanamichezo maarufu duniani, Christian Ronaldo na Pep Guardiola wameingia katika kundi la watu maarufu duniani waliochangia mapambano dhidi ya ugonjwa wa virusi vya corona.
Ronaldo, mshambuliaji wa Juventus, pamoja na wakala wake Jorge Mendes watatoa msaada wa vifaa kwa ajili ya vyumba vitatu vya uangalizi maalum hospitalini nchini Ureno.
Guardiola, kocha wa Manchester City ambaye alitwaa ubingwa wa Ulaya akiwa na Barcelona, ametoa dola 1.08 milioni za Kimarekani (sawa na takriban Sh2.5 trilioni) kuchangia mapambano dhidi ya ugonjwa huo ambao umeshaua zaidi ya watu 18,259 kote duniani tangu ulipoibuka mwezi Desemba.
Ronaldo na Mendes watatoa vifaa kwa ajili ya vyumba vyenye vitanda 10 katika hospitali ya Chuo Kikuu cha Lisbon Kaskazini (CHUN), ambayo ni umoja wa hospitali katika mji huo mkuu wa Ureno, kwa mujibu wa msemaji wa taasisi hiyo.
Hospitali hiyo ya CHULN ina vitanda 77.
Mendes na Ronaldo pia watatoa vifaa kwa hospitali ya Santo Antonio iliyo Chuo Kikuu cha Porto.
"Huu ni uwekezaji muhimu sana ambao unajumuisha zaidi ya mashine kumi za kupumulia na vifaa vingine muhimu," alisema Eurico Castro Alves, mkurugenzi wa idara ya upasuaji wa hospitali hiyo, akiongeza kuwa sehemu hizo za uangalizi wa karibu zitaitwa jina la mshambuliaji huyo.
Ronaldo amerejea kisiwani kwao ambako kuna watu 11 wenye maambukizi ya ugonjwa huo, Covid-19, kati ya watu 2,362 wenye maambukizi nchini Ureno. Nchi hiyo imeshapata vifo 30 vilivyotokana na ugonjwa huo unaoshambulia mfumo wa kupumua.
Ronaldo, ambaye alikuwa ameenda kumtembelea mama yake kisiwani humo, aliwekwa chini ya karantini baada ya mchezaji mwenzake wa Juventus, Daniele Rugani kugundulika kuwa na virusi hivyo baada ya kupimwa.
Mamlaka za kisiwani hapo zilisema Machi 12 Ronaldo alionekana hana dalili.
Nchini Hispania, Guardiola alitoa mchango kwa Chuo cha Afya cha Barcelona kwa ajili ya kununulia "vifaa vya tiba ambavyo kwa sasa vinakosekana katika hospitali za Catalonia," ilisema taasisi hiyo.
Mchango wake pia utatumiwa kununulia mashine za kupumulia na vifaa vya kujikinga kwa wafanyakazi wa hospitalini katika eneo hilo analotoka la kaskazini mashariki mwa Hispania.
Wakati huohuo, hospitali ya Barcelona imesema imepokea mchango kutoka kwa nahodha wa klabu ya Barcelona, Lionel Messi kusaidia vita hiyo.
"Asante sana Leo, kwa msaada wako na kuwajibika," ilisema hospitali hiyo katika akaunti ya Twitter.
Wakati hospitali hiyo haikusema ni kiasi gani ametoa nyota huyo, gazeti la kila siku la Mundo Deportivo limesema ametoa euro 1 milioni (sawa na takriban Sh3 trilioni).
Wakati ugonjwa huo ukisambaa duniani, Hispania ni moja ya nchi zilizo na maambukizi na vifo vingi, ikiwa ya tatu kwa idadi ya vifo baada ya kupoteza watu 2,696, huku ikiwa na maambukizi 40,000.

Advertisement