Ronaldo asikilizia uamuzi wa Uefa

Muktasari:

Ni kutokana na kadi nyekundu dhidi ya Valencia

Zurich, Uswisi. Mshambuliaji mahiri wa Juventus, Cristiano Ronaldo, atasubiria uamuzi wa kamati ya nidhamu ya Shirikisho la soka la Ulaya ‘Uefa’ kujua kama atafungiwa mchezo wa mmoja au mitatu.

Kamati hiyo itaketi Septemba 27, kuamua mambo kadhaa ikiwemo adhabu ya Ronaldo aliyetolewa nje kwa kadi nyekundu katika dakika ya 29, kwa madai ya kumvuta nywele Jeison Murillo wa Valensia bila kuwa na mpira.

Wakati sheria za nchi kama England adhabu ya kadi nyekundu ya moja kwa moja ni michezo mitatu, kanuni za Uefa zinatoa mwanya kwa kamati kuangalia mazingira ya kadi ikiwa ingeweza kusababisha madhara ndipo humsimamisha mechi tatu na kumtoza faini.

Hata hivyo marudio ya video yanaonyesha kuwa hakukuwa na uvunjifu wa Amani na Ronaldo anajitetea kuwa alienda kumgusa kichwani Murillo akimtaka anyanyuke badala yake mchezaji huyo akajidau kuugulia maumivu hadi mwamuzi alipomuona na kushauriana na msaidizi wake ndipo akatoa kadi nyekundu ya moja kwa moja.

Timu hizo zilikutana katika mchezo wa kwanza baina yao wa Ligi ya Mabingwa Ulaya na iwapo adhabu hiyo itaongezwa ataukosa mchezo mwingine wa kundi H, dhidi ya timu yake ya zamani Manchester United.

Hiyo ilikuwa kadi nyekundu ya 11 kwa Ronaldo lakini ni ya kwanza kwake katika Ligi ya Mabingwa Ulaya, iwapo adhabu haitaongezwa basi ataukosa mchezo ujao tu dhidi ya Young Boys ya Uswisi utakaopigwa mjini Turin.

Licha ya kadi hiyo nyekundu kwa nahodha huyo wa Ureno, wachezaji wenzake walipambana na kufanikiwa kuipa Juventus ushindi wa mabao 2-0 mabao ya penalti yakifungwa na Miralem Pjanic.