Rungu la TCU laishukia SMMUCo, yataka wanafunzi wahamishwe

Friday November 9 2018Katibu Mtendaji wa TCU) Profesa Charles Kihampa

Katibu Mtendaji wa TCU) Profesa Charles Kihampa 

By Kalunde Jamal, Mwananchi

Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefuta usajili wa kituo cha Chuo Kikuu Kishiriki cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (SMMUCo) na kuamuru wanafunzi wote wanaoendelea na masomo wahamishwe.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Novemba 9, 2018, Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa amesema mbali ya kufuta usajili wa chuo hicho, imeamriwa pia wanafunzi wote wanaoendelea na masomo wahamishiwe katika kampasi kuu ya chuo hicho iliyopo Masoka mjini Moshi mkoani Kilimanjaro.

Amesema TCU imezuia udahili wa wanafunzi wapya na kuamuru kuhamishwa mara moja kwa wanafunzi wa shahada ya kwanza wanaoendelea na masomo kwa mwaka 2018/19 katika programu tisa katika vyuo vikuu vinne.

Profesa Kihampa amesema zuio hilo linawahusu wanafunzi wote wanaosoma katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba na Teknolojia (IMTU) Dar es Salaam programu ya shahada ya tiba na upasuaji, shahada ya sayansi na uuguzi.

Amesema pia wanafunzi wote wanaosoma programu ya udaktari wa binadamu kutoka Chuo Kikuu Kishiriki cha Askofu Mkuu James (Ajuco), kilichopo Songea mkoani  Ruvuma watahusika.

Ametaja programu nyingine zilizozuiwa udahili kutoka SMMUCo Moshi kuwa ni za shahada ya sanaa na mawasiliano ya umma, na sanaa na utawala.

Amefafanua pia kuwa wamezuia udahili kwa wanafunzi wanaosoma programu za shahada ya elimu na mahitaji maalumu (sanaa), shahada ya elimu na mahitaji maalumu (sayansi), shahada ya sayansi na elimu na shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Kumbukumbu ya Sebastian Kolowa (Sekomu), Lushoto-Tanga.

Advertisement