Rwanda na Tanzania yaileta mapema vita ya Yondani, Kagere

Thursday October 10 2019

 

By OLIPA ASSA

Dar es Salaam. Kazi itakuwepo kati ya Kelvin Yondani na Meddie Kagere watakapokutana katika mechi ya kirafiki ya kimataifa baina ya Tanzania na Rwanda, itakayopigwa Oktoba 14, jijini Kigali.

Taifa Stars itacheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Rwanda ikiwa ni sehemu ya maandalizi yake ya mechi dhidi ya Sudan ya kufuzu fainali za CHAN, nayo Amavubi ikijianda kwa mechi dhidi ya Ethiopia ya kufuzu kwa fainali hizo za mwakani Cameroon.

Mchezo huo utatoa nafasi kwa Yondani na Kagere kukutana mapema zaidi msimu huu kabla ya mechi ya watani Yanga na Simba itakayochezwa mwakani.

Kagere ni mshambuliaji tegemeo Simba na timu ya taifa lake la Rwanda, wakati Yondani ni beki muhimu kwa Yanga na Taifa Stars, kukutana kwa wachezaji hao kunawakumbusha mashabiki mechi ya watani wa jadi, itakayochezwa Januari.

Kagere anaongoza kwa kufunga mabao sita katika Ligi Kuu Tanzania Bara pia ni mfungaji bora wa msimu uliopita akiwa na mabao 23.

Beki wa Polisi Tanzania, Iddy Mobby aliitwa katika kikosi kilichopita cha Stars, alizungumzia ubora wa Yondani inatakuwa kuwa mshambuliaji mwenye roho ngumu kumpita beki huyo.

Advertisement

"Nimejifunza kitu kwa Yondani baada ya kucheza naye Stars ni beki makini na anafanya kazi yake kwa kujiamini, wakikutana na Kagere katika mechi ya kirafiki kutakuwa na ushindani mkali,"alisema.

Kipa wa Yanga na Stars, Metacha Mnata alisema Kagere ni straika mzuri lazima wawe na tahadhari kama safu ya ulinzi namna ya kumkaba kwenye mchezo wao wa kirafiki na Rwanda.

"Mchezaji mzuri ni yule anayejua ubora na udhaifu wa mpinzani wake, Kagere ni mpambanaji lazima akakabwe vyema ili tukashinde mchezo unaotuandaa kwa ajili ya mchezo na Sudan," alisema Mnata.

 

Advertisement