Sababu Simba kufungwa na Mbao hizi hapa

Muktasari:

  • Licha ya kuwa na safu inayoundwa na nyota wenye majina makubwa, Simba inaonekana kukosa mbinu za kupenya ngome imara au wanapokutana na wapinzani wanaojaza idadi kubwa ya wachezaji mbele ya lango.

Mwanza. Tatizo la kukosa umakini na ubunifu kwenye safu ya ushambuliaji limeendelea kuigharimu Simba kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara na kuanza kuiweka kwenye hofu ya kutetea ubingwa msimu huu.

Licha ya kuwa na safu inayoundwa na nyota wenye majina makubwa, Simba inaonekana kukosa mbinu za kupenya ngome imara au wanapokutana na wapinzani wanaojaza idadi kubwa ya wachezaji mbele ya lango.

Hilo limejidhihirisha katika mchezo wa jana dhidi ya Mbao ambao licha ya Simba kutawala dakika zote 90, ilishindwa kufurukuta mbele ya safu imara ya ulinzi ya Mbao iliyoongozwa na nahodha, David Mwassa.

Beki huyo na wenzake waliwabana washambuliaji watatu wa Simba, Emmanuel Okwi, John Bocco na Meddie Kagere ambao walishindwa kutumia uwezo wao binafsi kuwapita mabeki wa Mbao au kutumia nafasi ambazo timu yao ilitengeneza kuifungia mabao muhimu kwenye mchezo huo.

Mbali na tatizo hilo, pia safu ya ushambuliaji inaonekana bado haina maelewano na mawasiliano mazuri ndani ya uwanja, jambo lililowafanya kushindwa kujipanga na kukaa kwenye nafasi sahihi wanaposhambulia.

Udhaifu wa Simba ulitumiwa vyema na Mbao ambayo pamoja na kucheza kwa kujilinda muda mrefu, ilifanya mashambulizi ya kushtukiza ya hapa na pale ambayo yalizaa matunda kwa kuiwezesha kuibuka na ushindi muhimu wa bao 1-0. Ni bao ambalo lilikuwa kama adhabu kwa Simba kwa kuwa lilitokana na mpira uliorudishwa vibaya na beki Shomari Kapombe kwenda kwa kipa wake Aishi Manula ambaye alichelewa kuokoa na kujikuta akimfanyia madhambi Pastory Athanas wa Mbao ndani ya eneo la hatari.

Kosa hilo lilimfanya mwamuzi Jonesia Rukyaa kumuonyesha kadi ya njano, Manula na kuizawadia penalti Mbao ambayo ilifungwa kwa ustadi na Said Khamis dakika ya 28.

Baada ya kuingia bao hilo, Simba ilionekana kucharuka na kupeleka mashambulizi langoni mwa Mbao, lakini hadi timu hizo zinakwenda mapumziko zilikuwa nyuma kwa bao moja.

Kipindi cha pili Simba iliongeza kasi ya kusaka bao la kusawazisha na ushindi huku ikifanya mabadiliko kwa kuwatoa Mohammed Ibrahim, Shiza Kichuya na nafasi zao kuingia Meddie Kagere na Rashid Juma ambao hawakuweza kuiokoa timu yao dhidi ya kichapo hicho.

Ushindi huo umeifanya Mbao ifute uteja iliyokuwa nao kwa miaka mitatu mbele ya Simba kwa kuwa katika mechi tano ambazo timu hizo zilikutana kwenye Ligi Kuu na Kombe la FA, Simba ilishinda mechi nne na kutoka sare moja.

Matokeo hayo pia yamefanya ndoto za Simba kumaliza ligi bila kufungwa zimeyayuka mapema baada ya msimu uliopita kushindwa kufanya hivyo dakika za lala salama ilipopoteza dhidi ya Kagera Sugar.

Msimu uliopita Simba ilipoteza mchezo mmoja kwa kufungwa bao 1-0 na Kagera Sugar mbele ya mgeni rasmi Rais John Magufuli kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, katika mchezo wa kukabidhiwa Kombe la Ligi Kuu.

Simba imepoteza mchezo wa jana, ikiwa tayari imeteremka uwanjani mara nne katika mashindano hayo msimu huu.

Kabla ya kuvaana na Mbao, timu hiyo ililazimishwa suluhu na Ndanda FC kwenye Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara.