Sababu ya Chirwa kukosa penalti Z’bar hii hapa

Thursday January 11 2018

 

By Thobias Sebastian,Mwananchi [email protected]

 Shujaa aliyetarajiwa kuleta heshima kwa Yanga kuipeleka fainali ya Kombe la Mapinduzi, Obrey Chirwa amepeleka kilio makutano ya Mtaa wa Twiga na Jangwani, Dar es Salaam.

Chirwa amegeuka shubiri kwa mashabiki wa Yanga baada ya kukosa penalti ya mwisho dhidi ya URA ya Uganda, katika mchezo wa nusu fainali uliochezwa jana kwenye Uwanja wa Amaan mjini hapa.

Mshambuliaji huyo aliwasili visiwani hapa jana asubuhi kutoka Dar es Salaam baada ya kutokuwemo katika kikosi muda mrefu.

Mchezaji huyo alikosa penalti ya tano iliyoamua ushindi wa mabao 5-4 baada ya URA kupata penalti zote tano baada ya timu hizo kutoka suluhu dakika 90.

Sababu za kukosa penalti

Pamoja na kucheza kwa dakika 37, mshambuliaji huyo kipenzi cha Yanga, hakupaswa kucheza jana kwa kuwa hakuwa fiti kimchezo kwasababu muda mrefu alikuwa kwao Zambia kumuuguza mama yake huku kukiwa na moja ya picha alizoweka katika mitandao ya kijamii akiwa analima mahindi shambani.

Baadhi ya mashabiki waliamini kuwa angekuwa mtazamaji, lakini kocha msaidizi wa timu hiyo, Shadrack Nsajigwa hakutaka kuingia ndani jana zaidi ya kusema ni uamuzi wa timu.

Mbali na kucheza, Chirwa hakutakiwa hata kukaa benchi la wachezaji wa akiba kwa kuwa kisaikolojia hakuwa mchezoni na hakustahili hata kupewa penalti kwani hata wakati anakwenda kupiga, hakuwa mwenye kujiamini ikilinganishwa na Papy Tshishimbi, Gadiel Michael, Hassan Kessy na Rafael Daud waliofunga penalti zao.

Penalti za URA zilifungwa na Mbowa Patrick, Kibumba Enoch, Shafiq Kagimu, Jimmy Kulaba na Brian Majwega.

Kauli za Watafiti

Watafiti wa soka nchini Norway wanasema kukosa na kufunga penalti kupo na kwamba mpiga penalti ana asilimia 92 ya kufunga kama ni penalti ya kawaida mchezoni, lakini kama penalti inataka ufunge matokeo yawe sare au kuipa timu ushindi (penalti ya kuamua) mpigaji ana asilimia 60 za kufunga.

Mchambuzi wa masuala ya soka, Pprofesa Geir Jordet wa Chuo cha Sayansi ya Michezo Norway kilichopo mjini Oslo anasema katika penalti tano tano, asilimia za kupata pia hupungua kwa wanaopiga kwani penalti ya kwanza kupata ni asilimia 86.6, penalti ya pili asilimia 81.7 na asilimia 79.3 kwa panalti ya tatu na kuendelea.

“Hii inahusisha zaidi suala la kisaikolojia,” anasema profesa Jordet.

Mtafiti mwingine, Rich Masters wa Taasisi ya Human Performance nchini Hong Kong, Masters, anasema kuwa wakati mwingine mpiga penalti anakosa kwa kuwa na hofu kama atapata ama la na mwisho wa siku anakosa.

Naye Mchambuzi wa vitabu, Mark Wilson nchini Uingereza anasema wakati mchezaji anakwenda kupiga penalti anawaza mengi: “Umetajwa kupiga penalti, unatoka katikati ya uwanja na mawazo, unachukua mpira, unauweka kwenye eneo lake la penalti, unarudi nyuma tayari kupiga, sasa hapo unawaza; hili ndilo tumaini la timu yangu, kila mmoja ananiangalia, sijui nitapata au nitakosa na mwisho wa siku anakosa.

Pambano lilivyokuwa

Yanga ilianza mchezo ikiwa imefanya mabadiliko ya wachezaji wanne waliocheza dhidi ya Singida United ulimalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1.

Lwandamina aliitazama mechi hiyo akiwa jukwaani akiendelea kuwaamini wasaidizi Shadrack Nsajigwa na Noel Mwandila tangu kuanza kwa mashindano hayo.

Yanga iliwapumzisha Edward Makka, Gadiel Michael, Yohana Nkomola na Rafael Daud na nafasi zao kujazwa na Papy Tshishimbi, Juma Mahadhi,Haji Mwinyi na Said Juma ‘Makapu.

Tofauti na Yanga, URA ilifanya mabadiliko mawili katika kikosi chao kilichocheza na Simba jana iliwaanzisha Ssemda Charles na Bokota Labama wakichukua nafasi za Peter Lwasa na Sseruyide Moses.

Hata hivyo, muda mrefu wa mchezo mpira ulichezwa eneo la katikati kwa kila timu kuonekana kuwa na hofu ya kutoruhusu bao la mapema.

URA ilijaribu mara kadhaa kupeleka mashambulizi langoni mwa Yanga, lakini ustadi wa mabeki wa timu hiyo uliisaidia kutowapa mwanya Waganda hao kupata bao.

Moja ya shambulizi ilitokea dakika ya 10 ambapo kipa Youthe Rostand alilazimika kufanya kazi ya ziada kuokoa mkwaju wa faulo wa Brian Majwega ambao ulipatikana baada ya Haji Mwinyi kufanya madhambi.

Yanga ilijaribu kuamka na kuanza kushambulia kwa zamu na URA lakini safu yake ya ushambuliaji ilionekana kukosa uelewano na kuwapa mwanya mabeki wa wapinzani wao kucheza kwa uhuru mkubwa.

Nusura Nkomola aipatie Yanga bao la ushindi dakika moja baadaye baada ya kupiga shuti kali nje ya eneo la hatari la URA.Taharuki ilitokea dakika ya 81 baada ya Lwassa kuunganisha kwa kichwa mpira uliopita nyavu za nje ambazo zilikuwa zimechanika na kuingia ndani ya bao la Yanga lakini mwamuzi alikataa bao hilo jambo lililosababisha azongwe na wachezaji wa URA.

Baada ya mchezo huo, nahodha wa URA, Allan Munaaba alisema kilichowapa mafanikio hadi wakaweza kucheza fainali ni nidhamu.     

Advertisement