Safari ya Simba SC yaishia DRC

Sunday April 14 2019

 

By Oliver Albert, Mwananchi

Dar es Salaam, Ule usemi wa Kila mtu ashinde kwao umeiadhibu Simba baada ya jana kukubali kipigo ha mabao 4-1 kutoka kwa TP Maszembe katika mchezo wa pili wa robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika uliofanyika Stade TP Mazembe Lubumbashi, DR Congo.

Suluhu waliyoipata Simba mchezo wa kwanza uliofanyika jijini Dar es Salaam ndio iliyowamaliza kwani TP Mazembe walionekana tangu mwanzo licha ya Simba kuwashtua kwa bao la mapema.

Matokeo hayo yanaifanya Simba sasa kurudi kumalizia viporo huku wakikunja kibindoni Dola 650,000 za CAF.

Katika mchezo wa jana, pamoja na kufungwa, kipa Aishi Manula alifanya kazi ya ziada kuipunguzia Simba kufungwa idadi kubwa ya mabao baada ya safu yake ya ulinzi kuonekana kupwaya m na kuruhusu mashambulizi mengi golini kwake.

Simba ndio ilikuwa ya kwanza kupata bao dakika ya pili tu ya mchezo lililofungwa na Emmanuel Okwi alimalizia pasi safi ya Haruna Niyonzima.

Kuingia kwa bao hilo kuliwaamsha wenyeji TP Mazembe ambao walilishambulia lango la Simba kama nyuki.

Mabao ya TP Mazembe yalifungwa na Kabaso Chongo dakika ya 21 kabla ya Meshack Elia kufunga dakika ya 38 baada ya mabeki wa Simba, Juuko Murshid na Zama Coulibaly kujichanganya. Tresor Mputu aliipatia timu yake bao la tatu dakika ya 62 na Jackson Muleka alihitimisha karamu ya magoli akifunga bao la nne dakika 75.

Advertisement