Salamba apewa angalizo

Muktasari:

Michuano ya Kombe la Mapinduzi ilikuwa kama kipimo kwa nyota wa Simba ambao hawaanzi kwenye kikosi cha kwanza cha kocha Patrick Aussems, akiwemo Adam Salamba lakini walishindwa kuonyesha kile kilichotarajiwa kwao.

ADAM Salamba anazidi kujipalilia makaa ya kukosa namba mbele ya Meddie Kagere, John Bocco na Emmanuel Okwi, kutokana na kushindwa kuonyesha kiwango katika michuano ya Kombe la Mapinduzi, ambalo Azam FC ndio mabingwa.

Awali Simba ilipeleka timu nzima kwenye michuano hiyo, siku mbili kabla ya mechi yao na JS Saoura kocha Patrick Aussems alikirejesha kikosi chake cha kwanza Dar es Salaam kujiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ya makundi.

Katika kikosi ambacho alikirudisha Dar es Salaam, Salamba hakuwepo ambapo alikuwa na nafasi kubwa kuanza kwenye mechi za Mapinduzi ambazo zilikuwa zinaendelea, lakini alishindwa hata kutikisa nyavu za wapinzani wao.

Kocha wa zamani wa Njombe Mji, Mlage Kabange amezungumzia hilo na kumtaka Salamba kuongeza juhudi lasivyo atakuwa anasubiri sana mbele ya Okwi, Kagere na Bocco.

"Kikosi ambacho kilibaki Mapinduzi kilipaswa kuonyesha uhai ili kujijengea kuaminiwa na kocha Aussems, ajabu walikuwa wanacheza kama watu walioridhika na wana uhakika wa namba ndani ya kikosi cha kwanza kitu ambacho si kizuri sana kwao.

"Mfano Salamba anacheza namba moja na watu wenye uwezo wa hali ya juu, ilikuwa nafasi yake kuonyesha kiwango cha juu kwenye michuano ya Mapinduzi,"anasema.