Samatta : Ndondo zimenibeba Anfield

Muktasari:

Samatta ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili kutoka Afrika Mashariki kufunga bao Anfield baada ya Victor Wanyama wa  Tottenham  Hotspur aliyefunga katika mchezo wa Ligi Kuu England msimu uliopita.

NAHODHA wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta juzi usiku aliandika rekodi barani Ulaya, lakini akafichua kuwa kelele za mashabiki wa Liverpool kwenye uwanja wa Anfield wala hazikumpa tabu.

Samatta alifunga bao pekee la Genk lililokuwa la kufutia machozi dhidi ya wenyeji Liverpool kwenye mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Bao hilo limemfanya aweke rekodi katika uwanja huo ambao umekuwa gumzo huko England kutokana na mashabiki wake kupiga kelele za kushangilia muda wote.

Samatta ameweka rekodi ya kuwa mchezaji wa pili kutoka Afrika Mashariki kufunga bao Anfield baada ya Victor Wanyama wa  Tottenham  Hotspur aliyefunga katika mchezo wa Ligi Kuu England msimu uliopita.

“Walikuwa wakipiga kelele muda wote, sio kwamba ni uwanja mkubwa sana kuliko vyote England, ila utofauti wake ni kuwa muda wote wao ni fujo, kiasi nikakumbuka shangwe la nyumbani katika mchezo dhidi ya Uganda,” alisema.

“Akili yangu niliekeza katika mchezo zaidi, sikutaka kutawaliwa na kelele za uwanja huo. Tulicheza vizuri kama timu na ndio maana baada ya kutanguliwa tuliweza kutoka nyuma kwa kusawazisha.”.

Samatta alisema, “bao langu halikuwa na msaada kwa sababu tulipoteza, lakini binafsi kufunga Anfield imenijengea kujiamini zaidi na kuona inawezekana kupata mabao hata Italia ambako tutacheza na Napoli.”

Mchezo huo ulikuwa wa pili kwa Samatta kucheza dhidi ya  Liverpool ambapo katika mchezo wa kwanza uliochezwa Ubelgiji, nahodha huyo wa Stars alipachika bao lililokataliwa na teknolojia ya VAR wakati wakipoteza kwa mabao 4-1.

 M ASTAA WENGINE 

Katika vipindi tofauti, nyota mbalimbali waliowahi na wanaotamba kwa sasa Ulaya, waliwahi kuzungumzia ugumu wa kucheza katika uwanja wa Anfield ambao ni wa 10 kwa ukubwa England.

Nyota hao ni Ryan Giggs, kocha wa timu ya taifa ya Wales, ambaye kipindi akiichezea Manchester United alikaririwa akisema, “sijawahi kucheza katika uwanja mgumu kama Anfield.”

Wayne Rooney aliyeicheza naye kwa mafanikio Man United na Andrey Arshavin aliyekuwa Arsenal walidai changamoto ambayo ilikuwa ikiwasumbua Anflied ni fujo za mashabiki wa timu hiyo ambao ni kama walikuwa wakipiga kelele masikioni mwao.

MABAO YAKE

Mpaka sasa Samatta ameifungia Genk mabao manane msimu huu katika mashindano yote, yakiwemo mawili ya Ligi ya Mabingwa, akionekana pia kuwa hatari kwa kufunga kwa kichwa.

Katika mabao manne ameyafunga kichwa dhidi ya Liverpool, Salsburg kwenye Ligi ya Mabingwa na katika Ligi alifunga dhidi ya Waasland-Beveren na Mechelen.

Kupitia mguu wake wa kulia amepachika mabao matatu huku wa kushoto akiwa na bao moja.

“Kufunga inatokea kulingana na mazingira,” alisema Samatta akizungumzia aina yake ya mabao.

Msimu uliopita aliifungia KRC Genk mabao 23 katika ligi ambayo ni maarufu kama Jupiter Pro.

MSUVA AKUBALI

Mshambuliaji mwenza wa sammata katika kikosi cha Taifa Stars, Saimon Msuva ambaye anaichezea Difaa El Jadida, amempigia saluti akisema ameipeperusha vyema bendera ya Tanzania licha ya timu yake kupoteza kwa mabao 2-1. “Alicheza vizuri sana, kiukweli anastahili kupongezwa, kufunga Anfield, sio jambo rahisi,” alisema pacha huyo wa Samatta anayetesa kwa kuzifumania nyavu huko Morocco anakokipiga soka la kulipwa.