Kauli ya Samatta baada ya kucheza Ligi ya Mabingwa

Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya Tanzania 'Taifa Stars, Mbwana Samatta amesema licha ya kufungwa bado anajiona mwenye bahati kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza wa Kitanzania kucheza Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Katika mchezo huo uliocheza nchini Austria, KRC Genk anayoichezea Samatta waliopoteza dhidi  ya Red Bull Salzburg kwa mabao 6-2.
"Nimekuwa nikipenda kuwa mfano bora kwa wengine ndio maana nimekuwa nikijituma siku zote ili wanaochipukia wajifunze kitu. Nilikuwa nashauku ya kucheza Ligi ya Mabingwa ambayo miaka ya nyuma nikiwa nyumbani, Tanzania niliishia kuiangalia kwenye Televisheni tu," alisema Samagoal.
Nahodha huyo wa Taifa Stars alisema "Nilishindwa kushangilia bao kwa sababu tulikuwa nyuma kwa idadi kubwa ya mabao. Naamini tunanafasi ya kugeuza aina ya matokeo mabaya ambayo kila mmoja wetu ameumizwa nao katika mchezo unaokuja, ambao tutakuwa nyumbani."
Samatta alisema ulikuwa ni usiku wa kila mchezaji kwenye kikosi chao kichanga ambao alitamani kufanya kitu ili kuhakikisha timu inapata matokeo mazuri, lakini wenzao waliyatumia vizuri makosa ambayo walikuwa wakiyafanya.
Saimon Msuva na mastaa wengine wa Kitanzania, wamempongeza Samatta kufuatia rekodi hiyo na kusema huo ni mwanzo ambao nahodha huyo, ameufungua kwa Watanzania wengine.
"Sasa tumeona kama inawezekana, nampongeza sana rafiki yangu, Samatta," alisema Msuva ambaye anaichezea Difaa El Jadida ya Morocco.