VIDEO: Samatta afunguka wanaomponda mitandaoni

Muktasari:

Samatta alilazimika kuunganishia ndege yake ya kurejea Ubelgiji akiwa nchini Uturuki na kushindwa kurudi moja kwa moja Tanzania baada ya kumaliza majukumu yake ya mechi za kimataifa.

LICHA ya shutuma ambazo zimekuwa zikitolewa mitandaoni na mashabiki wa Taifa Stars kuhusu kiwango cha nyota wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta, staa huyo wa klabu ya Genk ya Ubelgiji amesema hana muda ya kuzijadili.

Samatta alitoa kauli hiyo alipoulizwa kuhusu kiwango chake katika mechi mbili zilizopita za Taifa Stars dhidi ya Guinea ya Ikweta na Libya ambapo mashabiki wamekuwa wakilalamikia kiwango chake kuwa kimekwenda chini katika timu ya taifa.

“Siwezi kuzungumzia kiwango changu binafsi badala yake napenda nizungumzie kuhusu timu. Tumepoteza mechi lakini hatujapoteza vita. Bado tuna nafasi na tutarekebisha makosa yetu katika mechi zijazo. Ni suala la timu zaidi kuliko mchezaji mmoja.” Alisema Samatta.

Wakati Samatta akisema hivyo, staa mwingine wa Stars anayecheza soka la kulipwa nchini Morocco katika klabu ya Difaa El Jadida, Simon Msuva ambaye amesifiwa kwa kiwango kizuri katika mechi mbili zilizopita amedai kwamba anachofanya ni kujaribu kutimiza majukumu yake uwanjani.

“Binafsi najaribu kutimiza tu ninachoambiwa kufanya uwanjani. Najaribu kujituma kwa sababu hili ni taifa langu. Tumejitahidi lakini matokeo hayakuwa mazuri katika mechi hii.” Alisema Msuva ambaye alifunga bao la kwanza katika pambano dhidi ya Guinea ya Ikweta huku akisababisha penalti katika pambano la jana dhidi ya Libya.

Stars iliyorejea leo usiku ilikubali kichapo cha mabao 2-1 dhidi ya Libya katika pambano la pili la kufuzu michuano ya mataifa ya Afrika yatakayofanyika nchini Cameroon mwakani ikiwa ni baada ya kuichapa Guinea ya Ikweta mabao 2-1 jijini Dar es salam Ijumaa iliyopita.

Wakati huo huo Samatta alilazimika kuunganishia ndege yake ya kurejea Ubelgiji akiwa nchini Uturuki na kushindwa kurudi moja kwa moja Tanzania baada ya kumaliza majukumu yake ya mechi za kimataifa.