Samatta ahakikishiwa namba Villa keshokutwa

London, England. Benchi la ufundi la Aston Villa limemhakikishia nahodha na mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, Mbwana Samatta nafasi ya kucheza katika mchezo wa Jumanne dhidi ya Leicester City kutokana na kiwango bora anachoonyesha mazoezini.
Kocha wa timu hiyo, Dean Smith alikaririwa na mtandao wa Sky Sports jana akisema kuwa licha ya Samatta kuonekana anapata wakati mgumu kuhimili mazoezi mazito ambayo amekutana nayo katika timu hiyo, haoni sababu ya kutompa nafasi kwenye mchezo dhidi ya Leicester City akiamini atakuwa chachu kwao kufanya vyema.

“Amefanya mazoezi na sisi Alhamisi na ameonyesha kiwango kizuri. Anahitajika kuendana na kasi na anafahamu kwamba kiwango cha mazoezi ni tofauti na ilivyokuwa Genk,” alisema.
“Kwa hiyo mazoezi yetu ni magumu na anatakiwa azoee kwa haraka.Ameshapata utulivu na ni mchezaji mwenye haiba nzuri na itakuwa jambo jema kumjumuisha kwa namna fulani. Ni miongoni mwa walio tayari kujumuishwa Jumanne dhidi ya Leicester City.”

Samatta alijiunga na Aston Villa kwa dau la Pauni 10 milioni (takriban Sh 30 bilioni) akitokea Genk ambayo aliifungia mabao 10 msimu huu.