Samatta aiteka Uturuki, Galatasaray yamtaka kumrithi Msenegal

Muktasari:

  • Mbali ya Galatasaray timu nyingine zilizoonyesha nia ya kumtaka Samatta ni pamoja na Leicester, Aston Villa, Burnley na Watford zote za England.

Dar es Salaam. Jina la Mbwana Samatta limeteka vichwa vya habari vya tovuti, youtube, mitandao ya kijamii na magazeti ya Uturuki tangu ilipotoka taarifa ya Galatasaray kumtaka mshambuliaji huyo Mtanzania kutoka Genk.

Mabingwa wa Ligi Kuu Uturuki, Galatasaray jana walituma wawakilishi wao wakiongozwa na mkurungezi Sukru Hanedar kwenda Ubelgiji kuzungumza na klabu Genk kuhusu uwezekano wa kumsajili Samatta.

Tangu kutoka kwa taarifa hiyo vyombo vya habari vya Uturuki vimeripoti taarifa hiyo kwa vichwa mbalimbali vya habari.

Mtandao wa Aol Belgian press: Galatasaray meets with Mbwana Samatta (Galatasaray wamekutana na Mbwana Samatta).

I Haber7.Co: Galatasaray found the striker in Belgium! (Galatasaray imepata mshambuliaji Ubelgiji!)

Ajanssp: Here are Mbwana Samatta's strengths and weaknesses - Sports News (Huyu ndiye Samatta ubora wake na mapungufu yake)

Liberty: Şükrü Hanedar in Brussels for Samatta - Breaking Sports News (Sukru Hanedar yupo Brussels kwa ajili ya Samatta)

Ensonhab: Galatasaray will make an offer for Samatta (Galatasaray itaweka dau kwa ajili ya Samatta)

Fotospor: Galatasaray reveals EUR 10 million for Mbwana Samatta (Galatasaray imeweka Euro 10mili kwa Samatta)

Hivyo ni baadhi ya vichwa vya habari vilivyotawala jana katika mitandao nchini Uturuki.

Viongozi wa Galatasaray wamefika Luminus Arena kwa lengo moja la kufanya majadiliano juu ya uhamisho wa mchezaji huyo.

Galatasaray wanamtaka Samatta nahodha wa Tanzania kwa dau la euro 10 milioni ili kuziba pengo la mshambuliaji Msenegal Mbaye Diagne anayetaka kuondoka katika klabu hiyo.

Genk ipo tayari kuuza Samatta kwa dau la lisilopungua euro10 milioni, lakini Galatasaray wanataka kupunguza dau hilo ili kumsajili nyota huyo.

Samatta bado anamkataba na klabu yake ya Genk unaomalizika 2021, ukiwa na thamani ya Euros12 milioni.

Hata hivyo, Waturuki hao wanataka kuuza Diagne kwa euro 13milioni ili sehemu ya fedha hizo ndiyo zitumike katika kumnunua Samatta.

Galatasaray inapewa nafasi kubwa ya kumnunua Samatta baada ya kuingia katika meza ya majadiliano na Genk, tofauti na klabu za Leicester, Aston Villa, Burnley na Watford ambazo hazijatuma maombi rasmini.

Galatasaray ni mabingwa wa Ligi Kuu Uturuki wapo chini ya kocha Fatih Terim wapo tayari kutoa euro 10milioni kwa ajili ya kumnasa Samatta.

Msimu uliopita, Samatta alifunga mabao 32 katika mechi 51 alizocheza katika klabu yake ya Genk na kuisaidia kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji.