Samatta amliza babake akienda Aston Villa

Dar es Salaam. Baba wa Mbwana Samatta, mzee Ally Pazi Samatta, amesema alitokwa na machozi wakati mwanaye huyo alipompiga simu jana na kumweleza kuwa yuko Uwanja wa Ndege akielekea England kwa ajili ya kufanya vipimo vya afya kabla ya kumwaga wino wa kujiunga na klabu ya Aston Villa.

Dili la mshambuliaji huyo kutoka KRC Genk ya Ubelgiji kwenda katika klabu hiyo ya Ligi Kuu ya England, limeleta mwendelezo wa matukio ya kijana huyo kumtoa machozi baba yake.

Kila hatua anayopiga kijana wake huyo inaonekana ni nzito sana kuivumilia na mzee huyo amekuwa akilizwa na kila anachokifanya.

Kabla ya kwenda Genk, Samatta alitokea katika klabu ya soka la mchangani ya Kimbangulile ya Mbagala, baadaye akatua African Lyon ya Ligi Kuu Bara, akajiunga na miamba ya soka nchini Tanzania, Simba na kisha TP Mazembe kabla ya kwenda Genk.

Katika matukio ya karibuni zaidi yaliyomtoa machozi Mzee Samatta ni alipofunga bao katika Ligi ya Mabingwa Ulaya wakati akiitumikia Genk dhidi ya Liverpool kwenye Uwanja wa Anfield Oktoba 23, mwaka jana na hata alipofunga ndoa na mpenzi wake wa siku nyingi, Neima, Agosti 10 mwaka jana.

Mzee Samatta alisema jana kuwa amempa mwanaye uzoefu wa namna ya kuendana na tabia za Waingereza ili aweze kufika mbali.

Alisema ana uzoefu na tabia za Waingereza, hivyo alimweleza mwanaye kuwasoma wenyeji wake ili kufahamu jinsi ya kuishi nao.

Mzee huyo alisema wakati anasoma kozi ya Redio Engineering nchini Marekani mwaka 1967 kulikuwa na marafiki zake walikuwa wanasoma Uingereza hivyo alikuwa anakwenda kuwasalimia na ikamfanya kujua tabia zao.

Alisema baada ya mwanaye kumpa habari za kutua Aston Villa, alimpa maneno ya hekima kwamba mbali na kumpima afya, wanaangalia pia na tabia za nje ya uwanja.

“Mwaka 1967 nikiwa masomoni Marekani, nilikwenda kuwatembelea marafiki zangu Uingereza kuna wakati nilikuwa nakaa wiki tatu ama mwezi, niliwasoma tabia zao zipo tofauti kidogo na nchi nyingine.

“Kuna rafiki yetu alikula kuku akaanza kuvunja vunja mifupa, akaulizwa unapovunja mifupa unadhani mbwa atakula nini, akaendelea na dharau zake kisha akaitupa chini.

“Kilichofuata akaitwa na uongozi wa chuo akafukuzwa kwamba haendani na tamaduni zao, ndio maana nikaamua kumsisitiza mapema kuwasoma wenyeji wake kwa umakini,” alisema.

Alikiri ilikuwa ndoto yake kuona mwanaye anacheza Ligi Kuu England akisisitiza kwamba, ndio sababu akamkataza ofa za timu za Russia ambazo zilikuwa tayari kumlipa dau kubwa.

“Hata Mbwana mwenyewe alikuwa na ndoto ya kucheza Uingereza maishani mwake, ninachomuombea ni kila kitu kiende sawa ili aweze kuanza kazi,” alisema.

Alifichua siri kwamba mtoto wa kwanza wa Mbwana Samatta anayeitwa Karim (5) kuna uwezekano mkubwa akampeleka shule za soka nchini humo.

“Tangu mwanzo alisema ‘nikifanikiwa kupata timu ya Uingereza mwanangu atakwenda kusoma huko’.

“Mtoto wake ni mchezaji mzuri anacheza namba 10 kama baba yake, naamini hata hilo litatimia kwa uwezo wa Mungu,” alisema.

Endapo dili lake likifanikiwa Samatta ataachana na Genk akiwa na rekodi ya kuvutia kwani katika mechi 191 alizocheza amefunga mabao 76 na ametoa pasi za mabao 20. Msimu huu katika mechi 28, ametupia mabao 10.