Samatta ampa shavu Okwi, Niyonzima

MCHEZAJI ghali zaidi wa Tanzania, Mbwana Samatta, anayekipiga Aston Villa ya England, amewataja Meddie Kagere na Emmanuel Okwi kuwa mastraika wake bora wa kigeni mpaka sasa.

Samatta ambaye ni nahodha wa Taifa Stars, amewataja Kagere ambaye ni Mnyarwanda mwenye asili ya Uganda na Okwi raia wa Uganda kwenye kikosi chake ‘first 11’ ya wachezaji wa kigeni wanaocheza na waliowahi kucheza Tanzania.

Kagere bado anaichezea Simba, Okwi alicheza kwa Wekundu hao wa Msimbazi na Yanga kwa sasa anacheza Misri katika Klabu ya Al Ittihad.

Mbali na hao, Samatta amemtaja Mghana Yaw Berko aliyezichezea Simba na Yanga miaka ya nyuma kuwa kipa wake bora, huku Mkenya aliyepita Azam FC, Ibrahim Shikanda akimweka beki ya kulia na beki ya kushoto ni Mnyarwanda mwenye asili ya DR Congo, Mbuyu Twite. aliyecheza Yanga.

Samatta ambaye ametumia mfumo wa mabeki wanne, viungo watatu na washambuliaji watatu yaani 4-3-3, katika beki ya kati amewataja Muivory Coast wa Simba, Pascal Wawa na Joseph Owino, raia wa Uganda aliyekuwa Simba, Azam FC na Lipuli FC.

Viungo ni Mkenya Jerry Santo aliyecheza Simba, kati Mzambia wa Simba, Clatous Chama kulia na Patrick Ochan, raia wa Uganda kushoto aliyecheza Msimbazi.

Mnyarwanda wa Yanga Haruna Niyonzima, atakuwa na kazi ya kuwasaidia washambuliaji mbele, Kagere na Okwi.

Samatta ambaye alianza kucheza soka African Lyon kisha Simba kwenye Ligi ya Tanzania, TP Mazembe ya DR Congo, Genk ya Ubelgiji na sasa Aston Villa yuko mapumzikoni England kupisha janga la corona.