Samatta awaongoza mastaa wa timu pinzani waliofunga Anfield

Friday November 8 2019

 

LIVERPOOL, ENGLAND. ANFIELD haujawahi kuwa uwanja mwepesi, asikuambie mtu. Kwa msimu huu, kwenye mikikimikiki ya Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya, Liverpool imeruhusu mabao tisa tu kutinga kwenye nyavu zake katika mechi ilizocheza uwanjani hapo.

Na ni mmoja tu aliyefunga mara mbili uwanjani hapo kwenye michuano hiyo iliyotajwa hapo juu, kiungo wa Arsenal, Lucas Torreira aliweka rekodi ya kuifunga Liverpool mara mbili mfululizo alipofanya hivyo kwenye Ligi Kuu England na kurudia kwenye mechi ya Kombe la Ligi.

Kwa maana ya mabao tisa iliyoruhusu Liverpool kufungwa uwanjani Anfield kwenye Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya, imecheza tisa imehusika na hivyo ndivyo ilivyokuwa.

Teemu Pukki – Bao la kufutia machozi (Ligi Kuu)

Kwenye mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu England msimu huu, Liverpool ilianzia nyumbani uwanjani Anfield ilipoikaribisha Norwich City na kuichapa 4-1, bao la kujifunga la Grant Hanley kisha Mohamed Salah, Virgil van Dijk na Divock Origi wakaongeza mengine kabla ya mapumziko. Kipindi cha pili, Norwich City ilipata bao moja, Teemu Pukki alipoifungia bao la kujifariji au kufutia machoni kwenye dakika ya 64.

Lucas Torreira – Bao la kufutia machozi (Ligi Kuu)

Advertisement

Agosti 28, Liverpool ilishuka tena uwanjani Anfield kuwakaribisha wababe wenzao wa Big Six, Arsenal kwenye mchezo wa Ligi Kuu England. Mechi hiyo ilikuwa moto kwelikweli, Liverpool iliipiga Arsenal 3-1 shukrani kwa mabao ya Joel Matip na Mohamed Salah, aliyefunga mara mbili, bao moja likiwa la mkwaju wa penalti. Lakini, dakika tano kabla ya filimbi ya mwisho Lucas Torreira aliifungia Arsenal bao la kujifariji na hivyo kuwa kwenye orodha ya wakali waliofunga uwanjani Anfield msimu huu.

Jetro Willems – Bao la kuongoza (Ligi Kuu)

Kwenye raundi ya kwanza ya Ligi Kuu England, Liverpool imeshamalizana na Newcastle United na mchezo huo ulifanyika Septemba 14 uwanjani Anfield, kikosi hicho cha Jurgen Klopp kilishusha kipigo cha mabao 3-1, Sadio Mane akifunga mara mbili na jingine alifunga Mohamed Salah. Lakini, kwenye mchezo huo, Jetro Willems wa Newcastle United ndiye aliyefunga bao la kwanza, akiiongoza Liverpool kabla haijasawazisha na kushinda.

Erling Braut Haland – Bao la kusawazisha (Ligi ya Mabingwa)

Oktoba 2, Liverpool iliikaribisha RB Salzburg uwanjani Anfield katika mchezo wa Kundi E wa Ligi ya Mabingwa Ulaya. Mechi hiyo ilikuwa ya funga nikufunge, mabao saba yakitinga wavuni, ambapo Liverpool ilishinda 4-3. Liverpool ilitangulia kufunga kupitia kwa Sadio Mane, kisha ikaongeza jingine kupitia Andrew Robertson na Mohamed Salah kufunga mara mbili kabla ya Erling Braut Haland kufunga bao moja kwa RB Salzburg, baada ya mabao ya wakali wengine Hwang Hee-chan ambaye alimtesa beki Virgil van Dijk na lile la Takumi Minamino. Haland alifunga kufanya iwe 3-3 kabla ya Salah kupiga chuma cha ushindi.

James Maddison – Bao la kusawazisha (Ligi Kuu)

Mechi nyingine kali kabisa kwenye Ligi Kuu England iliyopigwa Anfield msimu huu ni ile ya Liverpool ilipocheza na Leicester City, iliyopigwa Oktoba 5. Katika mchezo huo, ambao Liverpool ilikabiliana na kocha wake wa zamani Brendan Rodgers na mchezo huo, Sadio Mane alipiga chuma cha kwanza dakika 40 na kuiongoza Liverpool.

Lakini, kiungo James Maddison alikuja kuisawazishia Leicester City kwenye dakika 80 kwa bao maridadi kabisa kabla ya James Milner kufunga bao la ushindi kwa mkwaju wa penalti katika dakika za majeruhi (90+5).

Harry Kane – Bao la kuongoza (Ligi Kuu)

Ile kipyenga pyee, dakika ya kwanza tu, straika Harry Kane aliifunga Liverpool uwanjani Anfield kuifanya Tottenham Hotspur kuiongoza Liverpool kwenye mchezo wa Ligi Kuu England. Bao hilo la Kane lilidumu hadi dakika 52, ambapo Liverpool ilisawazisha kupitia kwa Jordan Henderson kabla ya Mohamed Salah kuja kufunga bao la ushindi katika dakika 75, Liverpool ikishinda 2-1, lakini Kane akiingia kwenye orodha ya waliotikisa nyavu za Anfield kwa msimu huu.

Mbwana Samatta – Bao la kusawazisha (Ligi ya Mabingwa)

Supastaa wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta amekuwa mchezaji wa nne kufunga bao uwanjani Anfield kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya hadi sasa msimu huu.

Lakini, pia ni mchezaji wa tisa kwa kwenye Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa moja kufunga uwanjani Anfield tangu msimu huu uanze. Staa huyo wa Genk, alifunga kuisawazishia timu hiyo kwenye mchezo wa Kund E, ambapo ulimalizika kwa wenyeji kushinda 2-1. Georginio Wijnaldum alitangulia kuifungia Liverpool dakika ya 14 tu kabla ya Samatta kusawazisha kwa kichwa matata dakika tano kabla ya mapumziko. Liverpool iliongeza bao la pili na la ushindi kupitia kwa Alex Oxlade-Chamberlain.

Wachezaji wengine

Kwenye michuano isiyohusu Ligi Kuu England na Ligi ya Mabingwa Ulaya, ambayo mechi zake zimepigwa Anfield na wachezaji kufunga, ikiwamo ile ya Kombe la Ligi, ambapo Torreira, Gabriel Martinelli, Ainsley Maitland-Niles na Joe Willock waliifungia Arsenal kwenye sare ya 5-5.

Advertisement