Samatta: naondoka zangu Genk, naenda England

WATANZANIA wamekuwa na kiu kubwa kumuona Samatta akikipiga katika Ligi Kuu ya England au Hispania, hasa katika klabu zenye majina.

Mashabiki wa Genk wanataka staa huyo ambaye ni nahodha wa Taifa Stars abakie kwao kwa ajili ya kucheza katika Ligi ya Mabingwa wa Ulaya msimu ujao. Baada ya kufunga mabao zaidi ya 30 katika michuano mbalimbali msimu huu Ulaya,

Samatta amegeuka lulu kwa klabu mbalimbali kubwa za Ulaya. Namuuliza kama anatarajia kuondoka mwishoni mwa msimu huu. “Ndiyo, nitaondoka mwishoni mwa msimu huu,” anajibu Samatta. Jibu lake linakata kiu ya haraka haraka kwa mashabiki wa soka. “Kuna klabu kama sita za England ambazo zinanifukuzia. Moja inanifukuzia sana na imekuwa ikipiga simu kwa wakala wangu kila siku,” anasema Samatta.

“Kwa sasa sipo katika nafasi nzuri ya kuelezea ni klabu gani lakini pia kuna klabu nyingine mbili kutoka Hispania ambazo zimekuwa zikiisaka saini yangu. Hata hivyo, mimi ndoto zangu ni kucheza katika Ligi Kuu ya England.”

anaongeza Samatta. Samatta anathibitisha kwamba kulikuwa na ofa kutoka katika klabu ya Cardiff katika dirisha la Januari lakini Genk waliitupa kapuni.

Vyombo vya habari vya England viliripoti kuwa dau lililotiwa kapuni ni Pauni 13 milioni. Wakala wake mwanamke anayeishi England ndiye ambaye anapokea ofa zote.

Endapo dili hilo lingekamilika, Samatta angekuwa mchezaji ghali zaidi Afrika Mashariki akivunja rekodi ya staa wa kimataifa wa Kenya, Victor Wanyama ambaye katika dirisha kubwa la majira ya joto mwaka 2016 alihamia Tottenham akitokea Southampton kwa dau la Pauni 10 milioni. “Niliambiwa tu na wakala wangu kwamba Cardiff walikuwa wananifukuzia, Fulham pia walikuwa wameweka ofa, lakini mambo hayo huwa nawaachia mabosi wa klabu na wakala wangu.

Mimi kazi yangu kucheza mpira tu.” anaongeza Samatta. Badala yake Cardiff waliamua kumnunua mshambuliaji wa Nantes ya Ligi Kuu ya Ufaransa, Emmiliano Sala ambaye kwa bahati mbaya alifariki kwa ajali ya ndege kabla ya kuanza kuitumikia klabu hiyo ya Wales, kitu ambacho kilileta majonzi makubwa kwa mashabiki wa soka duniani kote. Samatta anakiri kwamba moja kati ya sababu ya kuondoka kwake Genk ni kujaribu kukimbizana na umri wake. kwa sasa ana umri wa miaka 26 na Desemba mwaka huu atatimiza umri wa miaka 27.

Hana miaka mingi sana ya kucheza katika kiwango cha juu na ni bora aichukue nafasi ya kucheza England kuliko kucheza mechi chache za Ligi ya Mabingwa wa Ulaya na Genk. “Umri haurudi nyuma. Ni kweli kwamba kuna raha yake kucheza katika michuano ya Ligi ya Mabingwa. Hawa jamaa hawajacheza Ligi ya Mabingwa tangu mwaka 2011 enzi za akina De Bruyne najua wanataka nicheze msimu ujao lakini Ligi Kuu ya England ina heshima yake,” aliongeza Samatta.

Samatta amegawanyika katika hisia za kuwa mchezaji wa kwanza kutoka Tanzania kucheza katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Anaweza kufanya hivyo na Genk. Lakini pia ana hisia za kuwa mchezaji wa kwanza wa Tanzania kucheza katika Ligi Kuu ya England. Tukiwa katika Uwanja wa Luminus, nyumbani kwa Genk,

Samatta anakiri kwamba soka la England liko mbali zaidi kuliko soka la Genk. Kuanzia ushindani uwanjani hadi mambo mengine “Ligi Kuu ya England ni ligi ambayo tayari imepiga hatua kubwa sana kulinganisha na Ligi Kuu ya Ubelgiji. Ni ligi ambayo inapendwa na watu wengi duniani, Ligi inayoonekana sehemu kubwa duniani. Yaani kwa vitu vingi iko mbali. “Unachoweza kufananisha ni kama vile tu kwamba kila timu ina mashabiki wake. hapa mashabiki wa Genk ni wa Genk tu hawawezi kushangilia timu nyingine, pale England mashabiki wa Burnley ni wa Burnely tu hawawezi kushangilia Manchester United,” anaongeza Samatta.

Samatta anaamini kwa kucheza England atakuwa amefungua milango kwa wanasoka wengine wa Tanzania kucheza hapo pamoja na katika ligi mbalimbali za Ulaya. Anakiri kwamba wachezaji wa zamani walishindwa kufungua milango hii na ndiyo maana mambo yamekuwa magumu kwa wachezaji wa Tanzania.

“Mastaa wetu wa zamani wangecheza nje kwa mafanikio basi wangefungua milango, lakini wengi walitamba katika klabu za Tanzania kwahiyo wakatengeneza ndoto za vijana kucheza zaidi katika timu za Tanzania kama vile Simba na Yanga.” Anasema Samatta.

Kesho tunamalizia mahojiano yetu na Samatta akielezea safari ya Taifa Stars katika michuano ya Afcon pamoja na matazamio mbalimbali ya kikosi hicho ambacho yeye ni nahodha.