VIDEO: Samatta ndani ya jezi ya Aston Villa leo kuikabili Leicester nusu fainali kombe la ligi

Muktasari:

  • Samatta mwenye miaka 27 na Vardy mwenye miaka 33 ni washambuliaji wanaopewa nafasi kubwa kuamua matokeo ya mechi ya leo kati ya Aston Villa dhidi ya Leicester City.

Dodoma. Wakati Tanzania ikisubiri kwa hamu kumuona nahodha wao Mbwana Samatta akicheza mchezo wake wa kwanza Aston Villa, Kocha Dean Smith ana lake jambo lake kichwani.

Samatta aliyesajiliwa na timu hiyo kwa dau la Paundi 8.5 Milioni kwenye dirisha dogo la usajili unaoendelea, anatarajiwa kucheza mchezo wake wa kwanza kwa timu hiyo iliyocheza mechi nne zilizopita bila mshambuliaji wa kati kutokana na kuumia kwa aliyekuwa mshambuliaji wao Wesley Moraes.

Siku tano alizofanya mazoezi na wachezaji wenzake wa timu hiyo zimetosha kumfanya Samatta awe kwenye mipango ya mchezo wa leo dhidi ya Leicester City ambao ni nusu fainali ya pili ya kombe la ligi (Carabao) katika uwanja wa Villa Park baada ya mchezo wa kwanza uliochezwa King Power kumalizika kwa sare ya 1-1.

Ni mchezo huo ambao utaamua timu ya kucheza fainali katika uwanja wa Wembley dhidi ya mshindi wa mchezo mwingine kati ya Manchester City dhidi ya Manchester United utakaochezwa kesho Jumatano huko Etihad ambapo City walishinda mchezo wa kwanza kwa mabao 3-1.

Hata hivyo, Kocha Dean Smith kuelekea mchezo huo na uwezekano wa kumchezesha Samatta alisema anatarajia mshambuliaji huyo kuwapelekea fainali Wembley kwa kufanya makubwa leo, lakini akaweka tahadhari kwamba presha ya mchezo wa kwanza na ugumu wake unaweza kuathiri ubora wake.

"Naamini Samatta anaweza kutubeba na kutupelekea Wembley, wote tumeona matarajio yaliyopo ila kuna wasiwasi wa kuathiriwa na presha ya mechi hii japo ubora wake utatusaidia sana pale mbele," alisema Smith.

Akifafanua zaidi kwa kumlinganisha na Moraes aliyeumia, Smith alisema Samatta ni tofauti na Wesley kwa uwezo wake mkubwa wa kusimama vema ndani ya boksi kufunga magoli pamoja na umahiri wake wa kufunga mipira ya juu wakati Moraes sifa yake ni nguvu akibebwa na ukubwa wa mwili wake.

Upande wa pili Leicester City, Kocha Brendan Rodgers amethibitisha urejeo wa mshambuliaji wake Jamie Vardy aliyepona majeraha yake na kwamba atakuwepo kikosini leo dhidi ya Aston Villa akisisitiza anaweza kuanza ama akatokea benchi.

"Vardy atakuwepo kikosini amefanya mazoezi vema kuanzia wiki iliyopita kujiandaa na mechi hii tutatizama na kuamua kama ataanza ama atatokea benchi," alisema Rodgers.