Samatta njia ya mafanikio yafunguka upya

Muktasari:

  • Mfungaji bora wa KRC Genk msimu wa 2018/19, Mbwana Samatta amemaliza msimu wa Jupiler Pro League akiwa kinara wa mabao 23.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Samatta amekabidhiwa tuzo na kuvishwa Medali ya ubingwa wa Ligi Kuu Ubelgiji ‘Jupiler Pro League’ baada ya KRC Genk kupata sare ya 0-0 na Standard Liege katika mchezo wa mwisho wa msimu uliochezwa kwenye  Uwanja wa Luminus Arena.

KRC Genk imemaliza msimu ikiwa na pointi 52, mbili zaidi ya Club Brugge iliyoshika nafasi ya pili na zote mbili zitacheza Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao. 

Samatta alicheza kwa dakika zote 90, katika mchezo huo dhidi ya Standard Liege na baada ya mechi hiyo sherehe za ubingwa zilifuatia, wachezaji wa Genk wakikabidhiwa Medali za Dhahabu na Kombe.

Samatta alikabidhiwa tuzo yake mwanasoka bora Mwafrika anayecheza ligi ya Ubelgiji akiwa kinara wa mabao msimu huu akimaliza na jumla ya magoli 23 akifuatiwa na Hamdi Harbaoui wa Zulte-Waregem.

 


Samatta mwenye umri wa miaka 26, ameifungia Genk mabao 62 katika mechi 156 za mashindano yote tangu amejiunga nayo Januari mwaka 2016 akitokea TP Mazembe, DR Congo.

Katika ligi ya Ubelgiji pekee amefunga mabao 47 kati michezo 123 aliyoshiriki, kwenye Kombe la Ubelgiji amefunga mabao mawili katika mechi tisa na Europa League amefunga mabao 14 katika mechi 24.

Vilevile mshambuliaji huyo wa Tanzania aliifungia timu yake mabao matatu (hat-trick) katika michuano ya Europa league  dhidi ya klabu ya Uturuki ya Besikitas katika ushindi wa 4-2 nchini Uturuki.

Timu za KRC Genk na Club Brugge zimekatia tiketi ya kucheza Ligi ya Mabingwa 2019/20 kwa pamoja baada ya kumaliza ligi kwa zikichukua nafasi ya kwanza nay a pili.

Mbali na kuiongoza Genk kushiriki Ligi ya Mabingwa Uefa, pia ameongoza timu yake ya Taifa Stars kufuzu kwa mara ya kwanza Kombe la Mataifa ya Afrika baada ya miaka 39.