Senegal, Algeria zatinga fainali Afrika

Muktasari:

Senegal na Algeria zitacheza mchezo wa fainali ya Kombe la Mataifa Afrika, baada ya jana usiku kushinda mechi zao dhidi ya wapinzani wao.

Cairo, Misri. Senegal na Algeria zitavaana katika mchezo wa Fainali ya Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), baada ya jana usiku kushinda mechi zao.

Wakati Senegal iliichapa Tunisia bao 1-0, Algeria iliing’oa Nigeria kwa ushindi wa mabao 2-1. Mchezo wa fainali utachezwa Ijumaa wiki hii

Senegal imetingia fainali ya mashindano hayo kwa mara ya pili baada ya beki wa Tunisia Dylan Bronn kujifunga kwa mpira wa kichwa katika harakati ya kuokoa dakika ya 100.

Miamba hiyo ya soka ilikwenda muda wa nyongeza baada ya kutoka suluhu ndani ya dakika 90 za kawaida.

Senegal ilitawala mchezo kipindi cha pili ambako ilitengeneza nafasi saba kwa kupiga kiki, wakati Tunisia ilipiga mashuti mara mbili.

Katika moja ya matukio mshambuliaji nyota wa Liverpool, Sadio Mane alikosa bao akiwa katika nafasi nzuri ya kufunga.

Wakati Senegal ikitinga hatua hiyo, kiungo wa pembeni wa Manchester City, Riyad Mahrez alikuwa shujaa wa Algeria, baada ya kufunga bao la ushindi dakika ya 95.

Mahrez alifunga kwa kiki ya mpira wa adhabu aliyopiga kwa ufundi.

Awali, William Troost-Ekong alijifunga na kuipa Algeria bao la kuongoza kabla ya Odion Ighalo kufunga kwa mkwaju wa penalti.