Senzo aanika mipango ya kuipa utajiri Simba SC

Muktasari:

  • Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Senzo Mazingisa amedhamiria kuifanya klabu hiyo kuwa na mifumo bora ya kujiingizia kipato kupitia mashabiki na wanachama wake.

Dar es Salaam. Mtendaji Mkuu wa Simba SC, Senzo Mazingisa amedhamiria kuifanya klabu hiyo kuwa na mifumo bora ya kujiingizia kipato kupitia mashabiki na wanachama wake.

Akizungumza katika ofisi za magazeti ya Mwananchi na Mwanaspoti jijini Dar es Salaam, Mazingisa alisema lengo lake na kuifanya Simba kuwa klabu yenye uchumi imara kama zilivyo klabu nyingine kubwa Afrika.

Mazingisa alisema Simba inaweza kuitumia utaratibu wa kuanza kuthibitisha wanachama na matawi yaliyopo kujiingizia kipato na kuchangia kukua kwa uchumi wa Tanzania.

"Najua katika hili tunaweza kufanikiwa. Kama ni shabiki wa Simba, hutakiwi kupata bidhaa zetu kwa njia ya mkato, tutakuwa na utaratibu ambao utawafanya kupata bidhaa mbalimbali za klabu kupitia matawi, ni njia nyepesi," alisema.

Aliongeza, "Kwa kushirikiana na wanachama ina maana mashabiki wa Simba, wataachana na mambo ya kununua bidhaa feki hivyo klabu itajiingizia kipato kwa mfano, wanachama 1000 wamehusika kuchukua bidhaa, unadhani ni kiasi gani kitaingia? Sasa tunatakiwa kufika huko."

Katika mabadiliko hayo ya namna ya kuuza bidhaa zao, Senzo alisema kuna watu watapinga kutokana na manufaa binafsi ambayo wamekuwa wakijapata kupitia nembo ya Simba bila ya klabu hiyo kupata faida.

Kufikia malengo ya kuwa miongoni mwa klabu ya kiushindani Afrika, Senzo anaamini wanatakiwa kukua zaidi kiuchumi na hilo ndilo lililomleta nchini ili kuwa sehemu ya ukuaji huo.

"Napenda kuona Tanzania ikiwa na Ligi ya ushindani, inamaana kuwa zinatakiwa kuwepo zaidi ya klabu mbili zenye uwezo kiuchumi, tukifanikiwa hapo lazima hata timu ya taifa iwe bora," alisema Senzo.