Serengeti Boys yavuna mamilioni

Dar es Salaam. Ndoto za kufuzu Fainali za Kombe la Dunia kwa Vijana chini ya umri wa miaka 17 kwa timu ya taifa ya vijana wenye umri huo ‘Serengeti Boys’ zimeyeyuka baada ya kuondolewa kwenye fainali za Afrika (AFCON U17) zinazoendelea nchini.

Hata hivyo, licha ya kutolewa mashindanoni, Serengeti Boys itafuta machungu ya aibu ya kufanya vibaya nyumbani kwa kupata kifuta jasho ambacho ni kiasi cha Dola 50,000 (zaidi ya Shilingi Million 115) kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).

Kiasi hicho cha fedha ni sehemu ya mgawo ambao CAF wanatoa kwa timu shiriki za mashindano hayo kulingana na nafasi husika ambayo timu imeishia kuanzia kwenye hatua ya makundi hadi ile ya fainali.

Kwa mujibu wa muongozo wa mgawo wa fedha ambao CAF hutoa kwa timu kwenye mashindano inayosimamia, timu inayoshika mkia kwenye kundi katika mashindano ya Afrika kwa Vijana chini ya Umri wa miaka 17, inapata mgawo huo wa Dola 50,000.

Timu iliyomaliza nafasi ya pili kwenye kundi inapatiwa kiasi cha Dola 60,000 (zaidi ya Sh 138 milioni), fedha ambazo majirani zetu Uganda watapata baada ya timu yao ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17 ‘Uganda Cubs’ kumaliza kwenye nafasi hiyo katika Kundi A.

Bingwa wa mashindano hayo ataondoka na kitita cha Dola 150,000 (zaidi ya Sh 345 milioni), mshindi wa pili anapata kiasi cha Dola 100,000 (zaidi ya Sh 230 milioni) na timu mbili zitakazoishia nusu fainali, kila moja itapatiwa Dola 75,000 (zaidi ya Sh 172 milioni).