Serengeti kupewa makali Qatar

Dar es Salaam. Timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys inatarajiwa kuondoka nchini Machi 20 kwenda Doha, Qatar kuweka kambi ya mwisho kabla ya kushiriki Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) zilizopangwa kuanza Aprili 14 hadi 28, Dar es Salaam.

Akizungumza jana, Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Mirambo alisema kambi hiyo itamsaidia kuwapa makali wachezaji wake kabla ya kuanza fainali hizo.

Hivi karibuni Serengeti Boys ilishiriki mashindano maalumu yaliyoandaliwa na Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa Assist) yaliyofanyika mjini, Antalya, Uturuki na kucheza mechi tatu.

Timu hiyo ilianza kwa kufungwa bao 1-0 na Guinea kabla ya kupata ushindi wa 3-2 dhidi ya Australia na baadaye ilipoteza kwa kuchapwa mabao 5-0 ilipocheza na Uturuki.

Pamoja na matokeo hayo, mashindano hayo yaliwapa fursa wachezaji wa Serengeti Boys kujinoa na kurekebisha makosa kabla ya kuanza mashindano hayo.

Alisema mbali na kucheza mechi dhidi ya wenyeji, pia timu hiyo itacheza mechi za kujipima nguvu dhidi ya timu mbalimbali kutoka mataifa ya jirani na Qatar.

“Kambi hii itatoa fursa kwa wachezaji kujiandaa zaidi baada ya mashindano ya Uturuki. Wachezaji wanaendelea vizuri na mazoezi hapa nchini, kwa kifupi wameiva na wapo tayari kwa ajili ya mashindano.

“Kinachofanyika sasa ni kunoa makali yao zaidi huku tukirekebisha makosa yaliyoonekana katika mechi zilizopita. Tumejifunza mengi sana Antalya na kubwa zaidi morali ya wachezaji ipo juu wana kiu ya kufanya vizuri,” alisema Mirambo.

Serengeti Boys imepangwa Kundi A na Nigeria (Golden Eaglets), Angola na Uganda. Kundi B linaundwa na timu za Guinea, Cameroon, Morocco na Senegal.

Timu hiyo itaanza kampeni za kutwaa ubingwa wa Afcon dhidi ya Nigeria Aprili 14 kabla ya kupambana na Angola Aprili 17 na mechi ya mwisho itamaliza na Uganda. Fainali hizo zinatarajia kutumia jumla ya Sh3 bilioni