Shahidi afunguka kesi ya Malinzi

Muktasari:

  • Shahidi Hellen Adam ambaye alikuwa mlipaji wa TFF, alitoa maelezo hayo jana wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri, huku akiongozwa na Wakili wa Takukuru, Leonard Swai.

Dar es Salaam. Shahidi wa kumi katika kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka nchini (TFF), Jamal Malinzi na wenzake wanne ameieleza Mahakama jinsi alivyokuwa akifanya miamala ya pesa kutoka katika akaunti ya shirikisho hilo na kuziweka kwenye akaunti binafsi ya Malinzi

Shahidi Hellen Adam ambaye alikuwa mlipaji wa TFF, alitoa maelezo hayo jana wakati akitoa ushahidi wake katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri, huku akiongozwa na Wakili wa Takukuru, Leonard Swai.

“Nilikuwa napewa maagizo kutoka kwa mkurugenzi wa fedha, mhasibu mkuu na mhasibu msaidizi niandike hundi na niende kuchukua fedha kwenye benki husika,” alisema.

“Nikisharudi ofisini nilikuwa naelekezwa niweke kwenye akaunti ya Malinzi au kama ni ofisini Malinzi alikuwa anatoa maelekezo mtu wa kupokea fedha hizo mara nyingi alikuwa anamchukulia dereva wake Steven Mgunda au Milium Zayumba,” alidai Hellen.

Alidai kuwa kati ya fedha hizo alizolipwa Malinzi hakuwahi kuonyesha kiambatanisho chochote kinachoonyesha zilitumika kwa kitu fulani.

Mbali na Malinzi, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Katibu Mkuu wa zamani wa TFF, Mwesigwa Selestine (46), Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga (27), Meneja wa Ofisi TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya