Sheringham, Berbatov wamuibukia Solskjaer

Monday January 14 2019

 

Teddy Sheringham na Dimitar Berbatov jana walikuwa jukwaani katika mchezo ambao timu hiyo ilicheza na Tottenaham Hotspurs.

London, England. Nguli wa zamani Teddy Sheringham na Dimitar Berbatov jana walikwenda uwanjani kumpa tafu, Ole Gunnar Solskjaer katika mchezo ambao Manchester United ilishinda bao 1-0 dhidi ya Tottenham Hotspurs.

Sheringham na Solskjaer waliwahi kutengeneza pacha hatari katika kikosi cha Man United na wanakumbukwa zaidi mwaka 1999 katika mchezo wa Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya

Man United ikiwa nyuma kwa bao 1-0 dhidi ya Bayern Munich, ilitoka nyuma na kutwaa ubingwa kwa ushindi wa mabao 2-1 yaliyofungwa na Sheringham na Solskjaer ndani ya dakika mbili za mwisho kabla ya mpira kumalizika.

Lakini, jana nguli huyo alikwenda uwanjani kushuhudia nyota mwenzake akiwa kwenye benchi akiiongoza Man United katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa Uwanja wa Wembley.

Kwa upande wake Berbatov, aliyewahi kuzitumikia timu zote mbili Man United na Spurs kama ilivyokuwa kwa Sheringham, alikuwa jukwaani kushuhudia miamba hiyo ikitoana jasho.

Mshambuliaji kinda Marcus Rashford alikuwa shujaa wa Man United, baada ya kufunga bao hilo dakikaya 44 na kumpa Solskjaer ushindi wa sita mfululizo tangu alipotwaa mikoba ya Jose Mourinho.

Mastaa hao walikuwa kivutio jukwaani kutokana na rekodi zao kwa timu zote mbili ambako Sheringham alitamba Spurs kabla ya kutua Man United alikocheza kati ya mwaka 1997 na 2001.

Berbatov, ambaye kwasasa ni mchezaji huru, alivuma Spurs kati ya mwaka 2006 na 2008 kabla ya kujiunga na Man United kwa Pauni30 milioni.

Advertisement