Shikalo aacha majanga Kenya

KOCHA wa Bandari FC, Bernard Mwalala amelazimika kumsaka kipa kutoka nje ya nchi baada ya kumpoteza mlinda lango wake tegemeo, Farouk Shikalo aliyekwenda zake Yanga SC ya Tanzania.
Kipa huyo anategemewa kuwasili nchini wakati wowote kujiunga na timu hiyo ambayo leo Jumamosi itashuka kwenye Uwanja wa Nyayo, kuanza kibarua kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Ahly Shandi ya Sudan.
Huenda kipa huyo akakosa kuitumika timu hiyo leo, ila akapangwa kwenye mechi ya marudiano dhidi ya Ahly Alhli ugenini. Mpaka wakati huo kipa Michael Wanyika ndiye atakeyepewa majukumu hayo ya kulinfda goli la Bandari.
Licha ya kumpoteza Shikalo, Kocha Mwalala amesisitiza kikosi alichokisuka ni matata na kipo tayari kupiga shughuli msimu huu.
“Sina majeruhi yeyote kila mchezaji yupo seti naweza kusema nina kikosi dhabiti ambacho kipo tayari kuwakilisha taifa kwenye majukumu haya ya kimataifa,” Mwalala alisema.
Kuelekea msimu mpya, Mwalala amekirutubisha kikosi chake kwa kusaini wachezaji watatu kiungo Danson Chetambe kutoka Zoo FC, Alex Luganji (Nairobi Stima) na Cliff Kasuti (Sofapaka).
Akizungumzia usajili wake mpya, Mwalala alitoa utathmini wake wa ni kwa nini aliwafuata na anachotegemea kutoka kwao.
“Amekuwa akicheza vizuri sana kwenye misimu michache iliyopita na tunashukuru tulimnasa sisi sababu klabu kadhaa zilikuwa zikimfukuzia,” Mwalala alisema kumhusu Chetambe aliyepachika magoli 10 msimu uliopita.
Na kumhusu wing’a wa kulia Kasuti, Mwalala alihisi kuwa kocha wake wa zamani John Baraza alishindwa kumtumia vizuri.
“Kasuti hakuwa akipata muda wa kutosha wa mchezo katika klabu yake ya zamani ila ana uwezo mlubwa.”