Simba yaichapa Biashara United, Luis akifunga goli lake lakwanza

Saturday February 22 2020

 

By DORIS MALIYAGA

KIPENZI cha mashabiki wa Klabu ya Simba, Luis Miquissone, ameandika historia ndani ya kikosi hicho baada ya kufunga bao lake la kwanza katika mchezo wao dhidi ya Biashara United walioshinda mabao 3-1, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Luis alifunga bao hilo dakika ya 35, akipiga shuti kwa mguu wake wa kulia kutokana na pasi ya Jonas Mkude.
Bao hilo ni baada ya kinara wao wa mabao, Mnyarwanda Meddie Kagere kushindwa kufunga kwa penalti waliyoipata dakika ya 25.
Penalti iliyopigwa na Kagere mwenye mabao 14, ilidakwa vizuri na kipa wa Biashara United, Daniel Mgore ambaye alionyesha kiwango cha juu katika mchezo huo.
Simba walijipanga na kucheza kwa malengo ambayo yalizaa matunda dakika ya 68, baada ya Kagere kuunganisha krosi ndefu iliyopigwa na Luis kutoka upande wao wa kushoto na kuandika bao la pili.
Biashara United walipambana na kujibu mashambulizi dakika ya 71, wakipiga bao kupitia kwa Novatus Dismas aliyeunganisha mpira wa Atupele Green, ukaenda moja kwa moja kwenye lango la Simba ukamshinda kipa, Aishi Manura.
Simba waliandika bao la tatu dakika ya 87, likifungwa na Frances Kahata ambaye aliwachezesha shoo wachezaji wa Biashara United hadi kipa wao, Mgore.
Kutokana na matokeo hayo, Simba imeendelea kusonga mbele na kujihakikishia nafasi ya kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu  ambao utakuwa wa tatu mfulurizo na wa 20, tangu Ligi Kuu Bara ianze kuchezwa.
Watani wao Yanga ambao sasa wako nafasi ya nne, ndio wanaongoza kwa kutwaa kombe hilo mara nyingi ambayo ni 27.

Advertisement