Si bao la Makame tu, yapo mengi yenye utata duniani

Muktasari:

  • Kwa mujibu wa kanuni ya 11 ya sheria 17 za soka ambayo ni ile ya kuotea, kuna mambo matatu ambayo kwa namna yoyote ile yanaua sheria ya kuotea na bao likifungwa linakuwa halali.

Dar es Salaam. Wakati bao la Yanga dhidi ya Coastal Union likiibua mjadala kila kona, kumbukumbu zinaonyesha siyo tukio jipya kwani limewahi kutokea mara kwa mara duniani.

Utata wa bao la Abdulaziz Makame umetokana na mazingira ya uokoaji wa mpira ambao ulifanywa na beki wa Coastal akijaribu kuzuia mpira wa kichwa uliopigwa na kiungo huyo na namna mwamuzi msaidizi alivyotoa uamuzi usiokuwa sahihi.

Kwa kutazama haraka mpira huo haukuonekana kama umevuka mstari wa goli kama sheria ya 10 kati ya 17 za soka inavyoainisha, lakini marudio ya tukio hilo kwenye luninga yameonyesha Omari Salum aliokoa akiwa ndani ya goli la Coastal na ulishavuka mstari kwa juu.

Kitendo cha mwamuzi msaidizi, Credo Mbuya kunyoosha kibendera kuashiria wachezaji wa Yanga waliotea kabla ya kufunga na kukishusha kimechangia bao hilo kuonekana lenye utata.

Kwa mujibu wa kanuni ya 11 ya sheria 17 za soka ambayo ni ile ya kuotea, kuna mambo matatu ambayo kwa namna yoyote ile yanaua sheria ya kuotea na bao likifungwa linakuwa halali.

Mambo hayo ni mpira wa kurusha, pigo la golikiki na kona. Pengine Mbuya alikishusha haraka kibendera na kuanza kukimbilia kati, jambo lililompa uhakika mwamuzi wa kati, Abubakari Mtulo kutoka Mtwara kuamua kuwa ni bao halali.

Yapo matukio mengi ya utata kuhusu mabao ambayo yamewahi kutokea katika viwanja mbalimbali duniani kama ilivyo kwa bao hilo.

Mfano mzuri ni mechi ya watani wa jadi, Yanga na Simba iliyochezwa Machi 5, 2011 waliotoka sare ya bao 1-1 ambapo mwamuzi Oden Mbaga alijikuta katika wakati mgumu baada ya kukataa bao la Simba lililofungwa na Mussa Hassan ‘Mgosi’ na kisha kulikubali baada ya kutazama marudio kwenye luninga kubwa iliyopo uwanjani hapo.

Mgosi alipiga shuti lililogonga nguzo ya juu na mpira huo kudondokea ndani huku ukivuka mstari wa goli, lakini baada ya kudunda ulirudi uwanjani, tukio ambalo lilimfanya mwamuzi huyo na msaidizi wake kuamini haukuvuka mstari, lakini baada ya kuzongwa na wachezaji wa Simba waliomtaka atazame luninga, Mbaga alipuliza filimbi kuashiria ni bao.

Juni 27, 2010, shuti lililopigwa na Frank Lampard wa England liliokolewa wakati mpira ukiwa umeshavuka mstari wa goli, lakini mwamuzi Jorge Larrionda wa Uruguay hakupuliza filimbi kuashiria ni bao.

Tukio la kukataliwa bao hilo katika mchezo ambao England ilichapwa mabao 4-1 ndilo lilikuwa kiini cha kuanzishwa kwa teknolojia ya goli (VAR) inayomjulisha mwamuzi bao limefungwa au vinginevyo.

Mwaka 2000, kiki ya penalti ya nyota wa zamani wa Nigeria, Victor Ikpeba iligonga mwamba wa juu na kudundia ndani kabla ya kurudi uwanjani, lakini mwamuzi aliamuru kuwa imekoswa ingawa kihalali alikuwa amepata na mwisho wa mechi Nigeria ilifungwa 4-3 baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 katika dakika 120. Mwamuzi wa zamani ambaye alikuwa na beji ya kimataifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA), Oden Mbaga alisema si jambo la kushangaza mwamuzi au msaidizi kubadili uamuzi pindi anapobaini alikosea.

“Mazingira yanamruhusu mwamuzi kufanya kitu kama hicho, lakini ni lazima mpira uwe haujachezwa, hivyo kwa hicho alichofanya refa msaidizi ni jambo sahihi kwa sababu mpira hakuwa umeanza baada ya tukio hilo,” alisema.

“Kosa linakuwepo ikiwa tayari mpira umeshaanzishwa halafu ndio refa anasimamisha na kubadili maamuzi.”

Nahodha wa zamani wa Yanga, Ally Mayay alisema bao la Makame ni halali na halikuwa na utata. “Ukiangalia utamuona yule mchezaji aliyeruka kichwa kuokoa yuko ndani ya mstari goli,” alisema Mayay.