Siku 540: Manji avunja ukimya Yanga

Monday November 12 2018

 

By Charles Abel,Thomas Ng’itu [email protected]

Dar es Salaam. Baada ya ukimya wa siku 538, mfanyabiashara maarufu Yusuf Manji, ametegua kitendawili baada ya kuamua kurejea rasmi ndani ya Klabu ya Yanga katika nafasi ya Mwenyekiti.

Kurejea kwa Manji aliyetangaza kujiuzulu Mei 23, 2017 kulitangazwa jana na Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini wa Klabu hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Makao Makuu Mtaa wa Jangwani, Dar es Salaam.

“Kwenye mkutano mkuu ule wa wanachama, ilipigwa kura nani wanamtaka Manji arudi aendelee na uenyekiti? Wajumbe wote 4,500 walisema tunamtaka Manji arudi.

“Baada ya kikao kile, Baraza la Wadhamini tulikaa kikao tukakubaliana Manji aandikiwe barua. Tulimuandikia barua nimesaini mimi Mwenyekiti wa Baraza la Wadhamini. Majibu ya Manji yamekuja. Mimi ndiye niliyemuandikia barua kwa hiyo alipaswa aniandikie mimi.

“Manji amejibu barua kwa Kiingereza. Kifupi anasema nimepokea uamuzi wa wanachama wa Yanga kwa bahati mbaya kipindi ninachoandikiwa nipo kwenye matibabu. Tarehe 15 Desemba madaktari wangu wanasema nitakuwa nimekamilika. Kwa hiyo pamoja na kwamba nimerudi kama mwenyekiti, nitafanya kazi za kwenda ofisini kila mara kuanzia tarehe 15 Januari,” alifafanua Mkuchika.

Mkuchika alisema Baraza la Wadhamini limebariki kurejea Manji kwa mujibu wa barua aliyoandika kwasababu ni matakwa ya mkutano mkuu.

Alisema mchakato wa uchaguzi wa kuziba nafasi nyingine ambazo ziko wazi ni lazima na alisisitiza ufanyike ingawa ameshauri usimamiwe na Kamati ya Uchaguzi ya Yanga siyo Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Kuhusu angalizo la TFF kuwa uchaguzi wa nafasi ya mwenyekiti ni lazima ufanyike, Mkuchika alisema baraza la wadhamini limeagiza Kamati ya Utendaji ya Yanga kutafuta suluhisho na shirikisho hilo ili kuondoa sintofahamu iliyopo.

“Tumewaita kamati ya utendaji wametujibu kuwa kamati ya uchaguzi wanayo. Hata kama isingekuwepo, kamati ya utendaji ilipaswa kuchagua kamati ya uchaguzi kwasababu, uchaguzi kusimamiwa na watu wa nje ni kuvunja Katiba ya Yanga,” alisisitiza Mkuchika.

Tamko la Mkuchika kuhusiana na kurejea kwa Manji, lilizua shangwe kwa umati wa mashabiki na wanachama wa klabu hiyo waliokusanyika makao makuu mapema klabuni hapo kusikiliza kile ambacho Baraza la Wadhamini lilipanga kuzungumza.

Kabla ya mkutano kuanza, shauku kubwa ya wanachama ilikuwa kusikia msimamo wa Baraza la Wadhamini juu ya sintofahamu iliyokuwa inaendelea kuhusu mchakato wa Uchaguzi Mkuu wa Yanga.

Dakika chache kabla ya mkutano kuanza, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Thobias Lingalangala alijikuta kwenye wakati mgumu kutoka kwa wanachama na mashabiki hao ambao walimvamia wakidai anatumika kuivuruga klabu yao.

Lingalangala ambaye juzi alitoa tamko la kuunga mkono mchakato wa uchaguzi kusimamiwa na TFF akiwa Kaimu Mwenyekiti wa Yanga, alilazimika kuokolewa na ‘makomandoo’ wa klabu hiyo waliomuwahisha ofisini ambako kulikuwa na kikao cha muda baina ya Baraza la Wadhamini na Kamati ya Utendaji kabla ya mkutano.

Katibu Mkuu wa Baraza la Michezo la Taifa, Alex Nkenyenge alisema hana taarifa za Yanga kumrejesha Manji, hivyo hawezi kuzungumzia suala hilo hadi atakapopata taarifa rasmi.

“Sijasikia kuhusu Yanga kumresha Manji, siwezi kuzungumza chochote kwa sasa hadi nipate taarifa rasmi,” alisema Nkeyenge.

Rais wa TFF, Walace Karia alisema suala la Yanga linaachwa kwa Yanga wenyewe, lakini akaomba atafutwe Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TFF, Wakili Ally Mtungahela kuzungumzia zaidi suala hilo. Wakili huyo alipotafutwa kwa simu yake haikupatikana hadi gazeti linakwenda mtamboni.

Advertisement